Habari za Kitaifa

Uamuzi wa Ruto kukumbatia RSF wachongea Kenya ikawekewa vikwazo na Sudan

Na  ANTONY KITIMO March 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UUZAJI wa chai ya Kenya nchini Sudan umepungua mno huku vita vikichacha katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Vita hivyo vimeathiri pakubwa mauzo ya chai katika mnada wa Mombasa.Mnamo Alhamisi, serikali ya kijeshi ya Sudan ilitangaza kuwa haitaruhusu tena chai, kahawa na bidhaa zingine za Kenya kuingia nchini humo.

Hatua hiyo ni kisasi cha kupinga uamuzi wa serikali ya Rais William Ruto kukaribisha wanachama wa kundi la Rapid Support Forces (RSF), ambalo limekuwa likipigana na jeshi la Sudan tangu mwaka 2023.

Taarifa kutoka Wizara ya Biashara na Ugavi ya Sudan ilisema: “Sudan imeamua kusitisha uagizaji wa bidhaa zote kutoka Kenya kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu mara moja.”

Chai ilikuwa bidhaa kuu ya Kenya inayouzwa Sudan ikiingiza takriban Sh1.9 bilioni mwaka 2022 kabla vita kuzuka nchini humo.Kufuatia machafuko hayo, mauzo imekuwa ikishuka kila mwaka.

Mwaka 2023 Kenya iliuza chai ya thamani ya Sh1.3 bilioni, kiwango ambacho kilizuka hata zaidi 2024.Serikali ya Sudan ilishutumu hatua ya Kenya kukaribisha RSF ikisema ni uhasama dhidi ya watu wa Sudan, na kuapa kuchukua hatua ikiwemo kupiga marufuku chai ya Kenya.

Sudan ni miongoni mwa masoko 10 bora ya chai ya Kenya – ya pili bora barani Afrika baada ya Misri – na mgogoro huo unaweza kuathiri mno biashara baina ya nchi hizo mbili.

Duru za kidiplomasia zilidokezea Taifa Leo kuwa Kenya haitaki tena kuunga mkono serikali mbili zilizo msambamba nchini Sudan, na badala yake inataka pande zote husika kushiriki mazungumzo ya kupata suluhisho la kisiasa kwa vita hivyo.Mwaka jana chai ya Kenya iliuzwa nchi 96 duniani, ikilinganishwa na mataifa 92 mnamo 2023. Pakistan ilibaki kuwa soko kuu ikiagiza kilo 206.27 milioni — asilimia 34.7 ya mauzo yote.

Mapema mwezi huu, wauzaji wa chai ya Kenya walielezea wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kutokana na mzozo wa Sudan.

Serikali ya Sudan ilisema kuwa hatua ya Kenya kuwakaribisha RSF ni uhasama dhidi ya watu wa Sudan na ikaapa kuchukua hatua zote zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku chai ya Kenya.

Sudan ni miongoni mwa masoko 10 bora ya chai ya Kenya, na mgogoro huu unaweza kuwa pigo jambo ambalo litaathiri mno biashara. Maafisa katika mnada wa chai Mombasa walisema wiki hii kuwa vita nchini Sudan ndicho kiini cha kushuka kwa mauzo, kuashiria jinsi hali ya usalama inavyoathiri biashara katika kanda ya Afrika Mashariki.