Dimba

Kenya Police, Tusker na Gor Mahia unyounyo mbio za kushinda Ligi Kuu

Na CECIL ODONGO March 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINYANG’ANYIRO cha ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) kilipamba moto kileleni Kenya Police, Tusker na Gor Mahia zikishinda mechi zao wikendi na kuendelea kufukuzania taji la msimu huu.

Jumamosi, Kenya Police ilipepeta Murang’a Seal 3-1 katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos huku Gor Mahia ikaonyesha mchezo ulioenda shule kwa kuilemea Bandari 2-0 uwanja wa Dandora jijini Nairobi.

Ijumaa, wanamvinyo wa Tusker walilemea Posta Rangers 2-1 katika uwanja huo wa Dandora.

Katika uwanja wa Dandora hapo Jumamosi, Gor ilipata mabao yake kupitia Alpha Onyango na Chris Ochieng’ ukiwa ushindi wa tatu kwa kocha Sinisa Mihic tangu apokezwe mikoba hiyo Februari 3 mwaka huu.

Alpha Onyango wa Gor Mahia asherehekea kufunga bao katika mechi mwaka jana. Alisaidia Gor kupepeta Bandari, Jumamosi. PICHA | CHRIS OMOLLO

Chini ya Mihic, Gor iliipiga Mathare United 2-1 mnamo Februari 8 kabla ikatoka sare tasa na Tusker pamoja na Bidco mnamo Februari 16 na Februari 20 mtawalia. Kisha K’Ogalo ikazima Kariobangi Sharks 3-1 mnamo Machi 5.

Kocha Mihic raia wa Croatia alikuwa mwingi wa furaha jinsi kikosi chake kilidhibiti mechi, iwe ni katika ufungaji magoli au kuweka ulinzi imara.

“Hatutalegeza kamba hadi tushinde taji la KPL. Leo (Jumamosi) nimefurahishwa na jinsi vijana walisuka mechi na kulinda ngome yetu. Nimefurahia jinsi  tulifunga mabao yetu mawili kwa sababu yalitokana na ushirikiano murwa.”

Mjini Machakos, Police ilipata mabao yake kupitia Mohamed Bajaber aliyefunga mawili naye David Ishura akongeza lingine. Victor Haki alifutia chozi Murang’a Seal.

Katika mechi nyingine, KCB waliendelea pia kutia presha timu zilizo juu ya jedwali huku Kelvin Okumu na Francis Kahiro wakiwapa ushindi dhidi ya Ulinzi Stars.

Lilikuwa bao la 12 la Kahiro ambaye ameshuhudia ukame wa magoli. Wanajeshi wa Ulinzi waliliwazwa na goli la Joseph Ochieng’ baada ya kumegewa pasi na Boniface Muchiri.

Jedwali

Zikiwa zimesalia mechi 10 kabla ligi ifike tamati maafande wa Kenya Police wanaongoza msimamo wa jedwali na alama 45, Tusker inafuata na alama 44 huku Gor ikiwa nambari tatu na alama 42.

Wanabenki wa KCB wamejikusanyia alama 39 baada ya mechi 24 japo pia wamekuwa na matokeo mseto yaliyowaponza baada ya kuongoza KPL kwa wiki kadhaa mkondo wa kwanza.

Aidha, Ryan Ogam wa Tusker na Moses Shumah wa Kakamega Homeboyz wanaofukuzia tuzo ya Kiatu cha Dhahabu waliendelea kupata ukame wa magoli wikendi.

Ogam anayeongoza orodha ya wafungaji kwa mabao 15 hajacheka na nyavu sasa katika mechi saba mfululizo huku Shumah mwenye magoli 13 akikosa kufunga katika mechi tatu zilizopita za KPL.