Yaya ashtakiwa kuiba ‘miungu’ wa mwajiri wake
YAYA ameshtakiwa kwa kuiba “miungu miwili” ya mwajiri wake.
Rita Akinyi Yohana alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina, mnamo Jumatatu Machi 17,2025.
Alikana shtaka la kuiba “miungu” hao wa Bw Kapoor Mohit mnamo Machi 11,2025.
Mbali na “mungu” huyo, Akinyi, aliyesakama kizimbani kwa mawazo na kujishika tama ilibidi aitwe maradha kadhaa kabla ya kutika.
“Habari.Wewe ndiwe Rita Akinyi Yohana. Mbona huitiki jina lako linapoitwa. Unaelewa lugha gani? Kiingereza ama Kiswahili,” Bw Onyina alimwuliza mshtakiwa.
Huku akitazama kona ya ukuta wa sembule ya mahakama, akiwa na mwingi wa mawazo, Akinyi alimjibu hakimu akisema, “Naomba nisomewe shtaka kwa lugha ya Kiswahili.”
Akinyi alikabiliwa na shtaka la kuiba “miungu”wawili –Sanamu- (Ghanesh Statutes) , sarafu za kigeni ikiwa ni pamoja sarafu za India almaarufu Rupees (30,000) na Riale 100.
Miongoni mwa sarafu anazodaiwa kutoweka nazo, Akinyi, ni pamoja na Dola za Marekani (USD-$) 4,000, Sh31,050, sarafu tatu za dhahabu, pasipoti tano, vitambulisho, manukato,kadi za benki, kitabu cha hundi na pete mbili za dhahabu.
Thamani ya vyote vilivyoibwa ikiwa ni pamoja na miungu hao ni Sh1,103,599.
Mjakazi huyo pia alidaiwa aliiba mkoba.
Kiongozi wa mashtaka alieleza mahakama mshtakiwa alipatikana na baadhi ya vitu vilivyopotea kutoka makazi ya Bw Kapoor Mohit katika mtaa wa mabanda wa Kawangware.
Akinyi aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “atafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi.”
Bw Onyina alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000.
Hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kusikizwa.