Habari za Kaunti

Mahakama yakataa ombi la kufunga akaunti ya Benki ya Seneta Karanja

Na JOSEPH OPENDA March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SENETA wa Nakuru, Tabitha Karanja, alipata afueni baada ya mahakama kutupilia mbali ombi la kufunga akaunti zake za benki kufuatia madai ya matumizi mabaya ya Sh 8.3 milioni za bajeti ya ofisi yake.

Jaji Samuel Mohochi aliamua kwamba ombi hilo halikuwa na msingi, akisema kuwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) tayari zinafanya uchunguzi kuhusu suala hilo.

Jaji alisisitiza kuwa mahakama inapaswa kuingilia kati tu ikiwa taasisi za kikatiba zitashindwa kutimiza majukumu yao.

“Mahakama inapata kuwa ombi hili halina msingi na hivyo linatupiliwa mbali,” aliamua Jaji Mohochi katika uamuzi aliotoa Jumatatu, Machi 17, 2025.

Kesi hiyo iliwasilishwa na wanaharakati Simon Nasieku na Benson Macharia, ambao walimshutumu seneta kwa kutumia vibaya fedha za umma.

Walitaka karani wa Seneti azuiwe kutoa fedha zaidi kwa ofisi yake hadi pale ambapo ukaguzi huru wa matumizi ya fedha utafanywa.

Kulingana na walalamishi, Sh2.1 milioni zilikuwa zimetengwa kwa mishahara, Sh2.27 milioni kwa ushirikishaji wa umma, Sh2.33 milioni kwa utafiti na mafunzo, na Sh1.6 milioni kwa uchapishaji na matangazo.

Katika hati yake ya kiapo, Macharia alidai kuwa seneta huyo wa Nakuru alishirikiana na watu wengine ili kutekeleza udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kesi hiyo ilitaja Karani wa Seneti, meneja wa ofisi ya seneta, na Meneja wa Benki ya Equity kama washtakiwa. Wanaharakati hao waliitaka mahakama kutoa amri ya kufunga akaunti zinazohusishwa na ofisi ya seneta huyo.

Katika kujibu malalamishi yao, Seneta Karanja alikana kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha na badala yake akamlaumu meneja wa zamani wa ofisi yake, Samuel Nderitu, kwa matatizo yaliyokumba ofisi  hiyo.

Alidai kuwa kujiuzulu kwa Nderitu kulihusiana na usimamizi mbaya wa fedha unaoshukiwa kufanyika katika ofisi hiyo.

Karani wa Seneti, Jeremiah Nyegenye, pia alipinga kesi hiyo, akisema kwa kuwa EACC na PSC zilikuwa tayari zinafanya uchunguzi, mahakama haipaswi kuingilia kati kabla ya uchunguzi huo kukamilika.

Aliomba mahakama iache taasisi hizo zikamilishe uchunguzi wao. Jaji Mohochi alikubaliana nao.