Habari za Kitaifa

Ndindi Nyoro afunguka, alia kusalitiwa na Ruto

Na CHARLES WASONGA March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MBUNGE wa Kiharu, Ndindi Nyoro, ameonekana kujipata katika njia panda kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku akiacha mustakabali wake ndani ya muungano wa Kenya Kwanza ukining’inia.

Bw Nyoro, ambaye alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa karibu zaidi na Rais Ruto kabla na baada ya kuundwa kwa serikali ya Kenya Kwanza, sasa anaonekana kutengwa na uongozi wa muungano huo huku akichelea kujiunga na mrengo wa Bw Gachagua anayehimiza umoja wa wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya.

Hali hii ilidhihirika wazi wiki jana alipotimuliwa kutoka wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, nafasi ambayo ilikabidhiwa Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi wa chama cha ODM.

Akizungumza Jumanne, Machi 18, 2025 jijini Nairobi, Nyoro alisema hajazungumza na Rais Ruto tangu Oktoba mwaka jana, 2024 na hajawahi kuelezwa sababu halisi za kutimuliwa kwake.

“Kama binadamu, tuna hisia. Ni wazi kuwa kama binadamu nilihisi kusalitiwa kwa kupokonywa wadhifa huo, hali inayoibua maswali kuhusu uhalisia wa urafiki wa kisiasa,” alisema.

Wakati wa mchakato wa kumtimua Bw Gachagua kama naibu rais mwaka 2024, Nyoro alihusishwa na kambi iliyodaiwa kumtetea Gachagua, hali iliyozua minong’ono kwamba msimamo wake kisiasa huenda ulimgharimu nafasi yake katika uongozi wa Bunge.

Licha ya masaibu yake, mbunge huyo anasisitiza kuwa bado anamheshimu Rais Ruto na viongozi wote wa Kenya Kwanza.

“Mara ya mwisho kwangu kuongea na Rais William Ruto ana kwa ana ama kwa njia ya simu ilikuwa kabla ya Oktoba mwaka jana. Vile vile, sijawahi kuongea na viongozi wengine wakuu wa muungeno wetu wa Kenya Kwanza tangu wakati huo. Lakini sitaki tena kujadili musuala ya watu,” Mbunge huyo wa Kiharu akaeleza.

Licha ya kuonekana kutengwa kutokana na hatua yake ya kutounga mkono hoja hiyo, kisha akatimuliwa wiki jana, Bw Nyoro anasema angali anamheshimu Rais Ruto na viongozi wengine wa Kenya Kwanza.

“Bado naheshimu viongozi wote licha ya kwamba sikuelezwa sababu zilizochangia kutimuliwa kwangu kutoka wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti,” akasema.

“Hata hivyo, inafaa kuzingatiwa kuwa nilishikilia nafasi hiyo kufuatia mashauriano. Kwa hivyo, kabla ya uamuzi kama huo kufanyika majadiliano ya kina sharti yafanyike. Lakini sijawahi kufanya mazungumzo na kiongozi yeyote wa muungano wetu kuhusu kuondolewa kwangu,” Bw Nyoro akaeleza.

Kabla ya uhusiano wao kuanza kudorora, Bw Nyoro alikuwa mwandani wa karibu zaidi wa Rais Ruto kiasi cha kupigiwa upatu kuteuliwa kama mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Jana, Jumanne, Mbunge huyo aliwashukuru Wakenya kwa nafasi ya kuwahudumia kama mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti akieleza kuwa cheo hicho kimemwezesha kutangamana na raia katika pembe zote za nchi.

Mbunge huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), na anayehudumu muhula wake wa pili, alimtakia heri njema Bw Atandi ambaye alichaguliwa Jumatano wiki jana.

Kuhusu madai yaliyotolewa bungeni wiki jana kwamba alitumia nafasi yake kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kulitengea eneobunge lake mgao mkubwa wa fedha za maendeleo, Bw Nyoro alichelea kujibu madai hayo.

“Takwimu zote ziko na zinasema ukweli. Sitaki kujibu maovu na maovu. Sitaki kujibu matusi na matusi. Kama kiongozi sitakubali kuchokozwa kisha niingie kwenye mitego ya watu kama hao,” akaeleza.

“Kama kiongozi unafaa kuwa mwangalifu usije ukabebeshwa mzigo wa hasira kisha ukose mwelekeo kisiasa na kiutendakazi,” Bw Nyoro akaongeza.

Wiki jana kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa mrengo wa wachache Junet Mohamed walimkaripia vikali Bw Nyoro wakidai alielekeza katika eneobunge lake kiasi kikubwa cha mgao wa Sh12 bilioni za kufadhili shughuli ya ushirikishaji umma kuhusu masuala ya bajeti.

Pia, wamekuwa wakidai anahusiana na Bw Gachagua.

Kuhusu uhusiano wake na Bw Gachagua, Mbunge huyo alieleza hivi: “Kama kiongozi niko tayari kushirikiana na viongozi wote kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wetu.”

Alipotakiwa kuelezea tathmini yake kuhusu utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza ndani ya miaka miwili na nusu iliyopita Bw Nyoro alisema “yale yanayoonekana ndio muhimu sio yanayosemwa.”

“Nikikuuliza aliyoyasema Rais Mwai Kibaki mwaka 2006 hautayakumbuka. Lakini ukitembea katika barabara kuu ya Thika utayaona. Ukweli huonekana waziwazi,” Bw Nyoro akaambia wanahabari.