Habari za Kitaifa

Wakulima walia amri ya serikali kuhusu mbegu haijatekelezwa

Na VITALIS KIMUTAI na WAIKWA MAINA March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKULIMA nchini wanaendelea kununua mbegu za mahindi kwa bei ghali licha ya serikali kutoa amri kuwa bei hizo zipunguzwe.

Amri hiyo ilitolewa na Wizara ya Kilimo na ililenga kupunguza gharama ya kilimo na kuongeza uzalishaji. Wakulima kutoka kaunti za Narok, Bomet, Kericho na sehemu za Kaunti ya Nakuru wamelalamika kuwa bei mpya zilizopunguzwa hazipo.

Hali ni hiyo hiyo kwa wakulima kutoka Nyandarua na Laikipia ambao wamelalamikia bei ya juu ya mbegu na pembejeo nyingine za kilimo.

Kusini mwa Bonde la Ufa, wakulima ambao wana vipande vikubwa vya ardhi Kaunti ya Bomet wamekuwa wakinunua mbegu kutoka bohari ya Kampuni ya Mbegu ambapo bei zilizopunguzwa za serikali zipo.

Hata hivyo, wanajikuna kichwa kwa sababu wanagharimia usafiri wa mbegu hizo.

“Maduka ya mbegu bado yanauza kwa bei ya zamani kwa sababu wanasema hazina yao haijaisha na hawataki hasara. Wanasema wangefidiwa na serikali kabla ya kuamrishwa kuuza kwa bei ya juu,” akasema Mary Kones, mkulima kutoka Chemaner Kaunti ya Bomet.

Paul Towett, mkulima kutoka Kelunet, Kericho aliwataka serikali ihakikishe kuwa mbegu zinapatikana mashinani.

“Wakulima wanastahili kununua mbegu maeneo yao. Hakuna haja ya kununua mbegu na kuokoa Sh50 lakini unatumia Sh200 katika uchukuzi,” akasema.

Huku mvua ikiwa imeanza, wakulima wanajiandaa kupanda nafaka hasa katika ukanda wa Bonde la Ufa ambao ni ghala la taifa. Kukosa kutekelezwa kwa bei mpya kumesababisha wakilalamikia gharama ya upanzi.

Mnamo Februari 25, Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt Paul Ronoh alimwaamrisha Meneja Mkurugenzi wa Kampuni ya mbegu Sammy Chesiror apige marufuku kuongezwa kwa bei ya mbegu.

Chini ya amri hiyo pakiti ya kilo moja ya mbegu ingeuzwa kwa Sh210, kisha kilo mbili Sh420 na kilo 10 kwa Sh2, 100. Pakiti ya kilo 25 ingeuzwa kwa Sh5, 250.

“Tulinunua pakiti ya kilo mbili kutoka Kampuni ya Mbegu Sh580. Kuziuza kwa Sh420 kuna maana kuwa tutapata hasara ya Sh160 kwa kila pakiti,” akasema muuzaji wa mbegu kutoka Kericho.

Kwa sasa pakiti ya kilo mbili ya mbegu inauzwa kwa Sh620 lakini kwenye kaunti za Nyandarua, Laikipia na Narok inauzwa kati ya Sh610 na Sh700.

“Nilikuwa nategemea kupanda mahindi kwenye ekari tano ya ardhi. Hata hivyo, kutokana na bei ya juu mbegu nimepunguza hadi ekari tatu,” akasema.