Habari za Kitaifa

Wakazi ‘walivyosafishwa’ na mvua wakielekea gangeni matatu zikiongeza nauli

Na SAMMY WAWERU March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAENEO kadha ya nchi asubuhi ya kuamkia Jumatano, Machi 18, 2025 yalishuhudia mvua, wengi wakilazimika kuvumilia manyunyu ya mvua kuelekea kazini.

Hii ni kutokana na mvua inayoendelea kunyesha sehemu tofauti nchini.

Mitaa mbalimbali Kaunti ya Nairobi, ilishuhudia mvua wakazi wakielekea kazini wakiwa wamelowa maji.

Kwa mfano, mtaa wa Zimmerman, Kasarani, Kahawa West, Githurai, Kayole, Dandora, kati ya mitaa mingine, wenyeji walistahimili mvua asubuhi.

Mojawapo ya barabara Zimmerman mvua ikiendelea kunyesha. PICHA|SAMMY WAWERU

Wahudumu wa matatu nao walitumia jukwaa hilo kuongeza nauli, kinyume na inavyotozwa.

“Kwa kawaida asubuhi, sisi hulipa nauli ya Sh80 ila leo imeongezwa hadi Sh100,” akasema mkazi wa Zimmerman.

Idara ya Utabiri wa Hewa Kenya, imesema mvua itaendelea kunyesha kwa muda wa siku saba mfululizo – kuanzia Jumatatu, Machi 17, hadi Jumatatu wiki ijayo, Machi 24.

Mtaro wa majitaka ukisafirisha maji ya mvua. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, inasema Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa (ikiwemo Kaunti ya Nairobi), kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi, na Nairobi, zinatarajiwa kuwa na mvua asubuhi katika maeneo machache.

Imekuwa desturi mvua inaponyesha asubuhi au jioni, maeneo ya miji hasa Nairobi wahudumu wa matatu kuongezea nauli.

Mitaa mingi Nairobi iliamkia mvua asubuhi ya Jumatano, Machi 19, 2025. PICHA|SAMMY WAWERU