• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
FORD-K, ANC na Wiper waungana dhidi ya ODM

FORD-K, ANC na Wiper waungana dhidi ya ODM

Na BENSON MATHEKA

VYAMA vitatu tanzu vya muungano wa NASA – Wiper, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) – vimeungana dhidi ya mshirika wake katika muungano huo ODM kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Embakasi Kusini.

Jana, vyama hivyo vilitangaza kuwa vitamuunga Bw Julius Mawathe wa chama cha Wiper dhidi ya Bw Irshad Sumra wa chama cha ODM kwenye uchaguzi huo.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, waliongoza viongozi wa vyama vyao na wale wa ANC kumsindikiza Bw Mawathe kuwasilisha stakabadhi zake za uteuzi kwa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Ninashukuru Ford Kenya na ANC kwa kuamua kumuunga Bw Mawathe. Huu haukuwa uamuzi wa Bw Wetang’ula peke yake, ni uamuzi wa chama cha Ford Kenya katika moyo wa ushirikiano,” alisema Bw Musyoka.

Bw Mawathe alipigwa jeki zaidi wakati aliyekuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 Paul Mutunga Mutungi alipomuunga mkono.

Chama cha Jubilee kilitangaza kuwa hakitawasilisha mgombeaji kwenye uchaguzi huo katika moyo wa muafaka.

“Huu muungano utaendelea kukua na kuwa mkubwa sana. Kwa sasa tunataka kudumisha amani na kumuunga Bw Mawathe kuhifadhi kiti chake,” alisema.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya ushindi wa Bw Mawathe kufutiliwa mbali na mahakama kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Sumra wa ODM.

ODM kilikataa wito wa Wiper wa kutowasilisha mgombeaji kwenye uchaguzi mdogo kikisema muungano wa NASA ulikufa. Pigo la kusambaratika kwa NASA lilibainika zaidi pale Kinara wa ODM Raila Odinga alipoamua kushirikiana na serikali ya Uhuru Kenyatta mnamo Machi mwaka jana.

“Ninahakika tutampatia Bw Sumra funzo kwenye uchaguzi huu,” alisema Bw Musyoka.

You can share this post!

3 ndani miaka 90 kwa wizi na unajisi

Ukosefu wa chakula walazimisha watoto kugura masomo

adminleo