Makala

WASONGA: Tulimpa Uhuru mamlaka, mbona awalilie wananchi kila mara?

February 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA huachwa na maswali chungu nzima wanapomsikiza na kumtizama Rais Uhuru Kenyatta akiwakaripia mawaziri wake kwa kutotekeleza majukumu yao inavyohitajika huku baadhi yao wakijihusisha katika siasa.

Pia imekuwa ada kwake kulalama kuwa baadhi ya mawaziri wake wanachelewesha utekelezaji wa mipango na miradi ya serikali, hususan, Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Nakubaliana na Rais Kenyatta kwamba utendakazi wa baadhi ya mawaziri haujaridhisha ilivyodhihirika katika siku za hivi karibuni.

Kwa mfano, wizara za Kilimo na Fedha hazijawahudumia wakulima wa mahindi ipasavyo kwa kufeli kuhakikisha kuwa wanalipwa pesa zao kwa wakati.

Usimamizi wa mpango wa elimu bila malipo, utekelezaji wa mtaala mpya wa masomo, usajili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya mafunzo ya ualimu na sekta ya elimu ya vyuo vikuu haujakuwa wa kuridhisha.

Na mwishoni mwaka jana sarakasi ilishuhudiwa katika makao makuu ya Wizara ya Michezo pale wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya walemavu walipopiga kambi katika afisi kuu ya wizara hiyo katika jumba la Kencom, Nairobi usiku na mchana wakiitisha marupurupu waliopasa kulipwa kwa kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Kombe la Dunia nchini Mexico.

Lakini kinaya ni kwamba mwaka huo, Waziri mhusika Rashid Echesa alitumia muda wake mwingi kulumbana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala huku akimpigia debe Naibu Rais William Ruto katika azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Lakini mbona awakaripie hadharani?

Badala ya Rais Kenyatta kulalamika kila mara kuhusu baadhi ya mawaziri wake, kile ambacho anafaa kufanya ni kuwafuta kazi wale ambao anahisi ni watepetevu au wanakiuka agizo lake kwamba wasijihusishe na siasa.

Kwa kulalamika mbele ya raia jinsi alivyofanya hivi majuzi mjini Kitengela, Rais alionyesha kukosa kutumia mamlakani aliyopewa na Katiba ya sasa ya kufanya mabadiliko katika serikali yake wakati wote anapohitaji kufanya hivyo.

Rais Kenyatta ndiye aliwateua mawaziri hao, bila kusaka ushauri kutoka kwa Wakenya. Hii ni kwa sababu Wakenya walimpa mamlaka ya kuunda serikali walipomchagua kuwa Rais wao mnamo 2017.

Matarajio ya wananchi ni kwamba serikali ya Rais Kenyatta itawahudumia kwa miaka mitano kulingana na ahadi ambazo aliwapa wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi uliopita.

Sio sawa kwa Rais kurejea kwa wananchi hao hao waliompa kura kwa wingi kulalama kuwa mawaziri ambao ni yeye aliwateua hawafanyi hili au lile.

Kwa mtazamo wangu, kile ambacho Rais Kenyatta anafanya, anapowasuta mawaziri wake hadharani bila kuwachukulia hatua zozote, ni kujiondolea lawama ambazo serikali yake inaelekezewa na wananchi

Anaonekana kuelekeza lawama hizo kwa mawaziri wake ambao, kimsingi, hawakupigiwa kura na Wakenya katika uchaguzi mkuu uliopita. Anayewajibika kwa Wakenya ni Rais wala sio mawaziri wake!

Tasnifu yangu ni kwamba, Rais Kenyatta atumie utulivu wa kisiasa ambao umekuwepo nchini tangu Machi 9, 2018 aliporidhiana kisiasa na Bw Raila Odinga kusuka upya serikali yake. Asipofanya hivyo haraka, ataondoka afisini 2022 bila kutekeleza mipango na miradi ya maendeleo aliyoahidi Wakenya.