Habari za Kitaifa

Gachagua akanyaga breki, apunguza ziara na mikutano ya wanahabari

Na CHARLES WASONGA Na BENSON MATHEKA March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amewaacha wengi na maswali baada ya kuonekana kupunguza makali yake ya kuishambulia serikali ya Rais William Ruto huku kiongozi huyo wa kitaifa akijiandaa kuzuru Mlima Kenya.

Aidha, mbunge huyo wa zamani wa Mathira amepunguza mwenendo wa kuhutubia wafuasi wake kila mara katika mikutano ya hadhara na kujitokeza mara nyingi kwa mahojiano katika redio na runinga za humu nchini.

Siku ya hivi punde kwa Bw Gachagua kuhojiwa na chombo cha habari ilikuwa Jumatatu asubuhi Machi 17, alipohojiwa na wanahabari wa redio na runinga ya Kameme, zinazotangaza kwa lugha ya Kikuyu.

Alichelea kutumia maneno makali dhidi ya Rais Ruto akisema kiongozi wa taifa yu huru kufanya ziara katika eneo la Mlima Kenya ila awahakikishie wananchi kuwa atakamilisha miradi iliyoanzishwa na rais mstaafu Uhuru Kenya na ile aliahidi yeye mwenyewe.

“Bila shaka watu wetu wamekatiza uhusiano wao wa kisiasa na Ruto. Lakini kama rais anakaribishwa kutembelea kwetu na awaelezee watu wetu ni lini atakamilisha miradi iliyoanzishwa na Uhuru. Vile vile, aeleze ni lini atatekeleza miradi aliyoahidi wakati wa kampeni,” akaeleza.

Miongoni mwa miradi ambayo Bw Gachagua anataka serikali ikamilishe ni ujenzi wa barabara ya MauMau ya umbali wa kilomita 500 inayopitia kaunti za Nyeri, Kiambu, Murang’a na Nyandarua.

Mingine ni ujenzi wa mabwawa kadhaa ikiwemo Karimenu iliyoko Gatundu Kaskazini, Kiambu.

Tangu alipotimuliwa afisini, Bw Gachagua amekuwa akitumia vyombo vya habari na mikutano mbalimbali, ikiwemo makanisa, kama majukwaa ya kuishambulia serikali ya Rais Ruto ambayo sasa imemshirikisha kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Februari 25, ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kuhojiwa katika kituo cha habari kisichotangaza kwa Kikuyu, alipojibu maswali kadhaa kutoka kwa wanahabari wa redio ya Kikamba, Musyi FM.

Inasemekana kuwa siku hizi Bw Gachagua ameamua kutumia muda mwingi kufanya mikutano na makundi mbalimbali ya watu wanaotembelea nyumbani kwake Wamunyoro, eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri.

Lakini hata wanaomtembelea Wamunyoro wanaonekana kupungua tangu Februari 22 alipotembelewa na Askofu Gerald Mureithi wa Dayosisi ya Mlima Kenya Magharibi.

Kutoka wakati huo ni Jumanne, Machi 25, 25 tu alipokutana na kundi la Wakenya wanaoishi ughaibuni nyumbani kwake Wamunyoro tofauti na awali alipokuwa akitembelewa na kukutana na jumbe tofauti na kuchapisha katika mitandao yake ya kijamii.

Japo Jumanne aliandamana na baadhi ya washirika wake wa dhati wakiwemo maseneta John Methu (Nyandarua), Karungo Thang’wa (Kiambu) na mbunge wa Embakasi ya Kati Mejja Donk, idadi ya wanasiasa wanaomchangamkia inaonekana kupungua..

Kwenye mahojiano kwenye kipindi cha “Fixing The Nation” katika runinga ya NTV, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba alimtaka mwanasiasa huyo kujizatiti ili aonekane kama kiongozi anayetetea masilahi ya Wakenya wote.

“Rigathi anapaswa kutambua kuwa Mlima uko naye. Hafai kuzungumza zaidi kuhusu masuala ya mlimani. Anapaswa kuonekana akitetea masilahi ya jamii zingine nje ya Mlima Kenya,” akaeleza mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wandani wa karibu wa Bw Gachagua.

Gachagua amewaahidi wafuasi wake kwamba atazindua chama kipya Mei 2025.

Awali, Bw Gachagua alitarajiwa kuzindua chama hicho mnamo Januari mwaka huu, alivyoahidi mwaka jana, lakini akabadilisha ratiba hiyo “ili kusubiri uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC”.

Lakini akiongea katika kanisa moja mjini Kitengela mnamo Machi 9 Bw Gachagua alifichua kuwa alichelewesha uzinduzi wa chama hicho kwa hofu ya kuvurugwa na serikali.

“Najua mnasema nimechelewa kuzindua chama. Lakini singetoa tangazo hilo Januari kwa sababu watu fulani walikiwekea chama hicho mitego fulani. Hii ndio maana niliamua kuchelewesha kidogo,” akaeleza.

Bw Gachagua alikariri kuwa wabunge, maseneta na madiwani wandani wake waliochaguliwa kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) wako tayari kukigura na kujiunga na chama hicho kipya.

Hata hivyo, kiongozi huyo amekuwa akishirikiana na viongozi wengine wa upinzani kama vile Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa (DAP-K) na Martha Karua wa chama cha Peoples Liberation Party (PLP)

Jumanne, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya alisema kiongozi huyo hajalegeza Kamba ukosoaji wake wa serikali bali “anafanya hivi kimkakati”.

“Sio lazima Rigathi aonekane kila siku kwenye runinga, kusikika katika redio au kufanya mikutano ya hadhari kuipiga vita serikali. Sio vizuri maadui wetu kisiasa kujua yale tunapanga kwa ushirikiano na wafuasi wetu kutoka pembe zote za nchini,” akaeleza.

Mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema “kutulia” kwa Gachagua ni kwa kimkakati akisema kuzungumza sana kunaweza kuwachosha wafuasi wake mapema kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Nafikiri ni hatua ya kimkakati kuepuka kuwapa wapinzani wake sababu ya kumshambulia. Kutulia kunampa nafasi ya kuwaacha wajitape akijipanga,” akasema.