Habari za Kitaifa

Uhaba wa vifaa vya Mpango wa Uzazi wawaweka wanawake hatarini

Na MERCY CHELANGAT March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NCHINI Kenya, uhaba mkubwa wa vifaa vya kupanga uzazi unawaweka mamilioni ya wanawake katika hatari, na kuwalazimisha wengine kutumia njia zisizo salama au kuacha kutumia mpango wa uzazi kabisa.

Serikali inahitaji Sh2.5 bilioni kila mwaka kufanikisha mpango huu, lakini kwa sasa inakabiliwa na pengo la ufadhili la asilimia 46, jambo linaloendeleza mgogoro huu.

Hali hii imezidi kuwa mbaya baada ya Serikali ya Amerika kusitisha usambazaji wa vifaa vya kupanga uzazi, ambavyo vilikuwa vikichangia asilimia 24 ya mahitaji ya Kenya.

Vituo vya afya vimeishiwa na njia muhimu za mpango wa uzazi, hasa kwa wanawake wa vijijini na maeneo yaliyo na uhaba wa huduma.

Kwa Alice Achieng, mama wa watoto watatu kutoka Kakamega, kupata njia ya mpango wa uzazi imekuwa safari ngumu.

Alipotembelea hospitali tatu za umma, alikosa dawa. Katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti, muuguzi alimwambia, “Hatujakuwa na vifaa kwa miezi kadhaa. Jaribu wiki ijayo.” Hatimaye, alilazimika kulipa mara tatu zaidi katika kliniki ya binafsi.

Kulingana na Sham Musyoki wa Marie Stopes International Kenya, kumekuwa na uhaba wa vifaa hivi kote nchini kwa miezi sita, huku sindano na vipandikizi vikiwa miongoni mwa vilivyoathirika zaidi.

“Matokeo yake yatakuwa ongezeko la mimba zisizopangwa, wanafunzi kuacha shule, na ongezeko la utoaji mimba usio salama, ambao unaweza kusababisha vifo,” alisema.

Wataalam wanalaumu pengo la ufadhili linalotokana na kujiondoa kwa USAID. Wanasihi wanawake kutumia njia za muda mrefu za mpango wa uzazi ili kupunguza athari. Serikali pia inaombwa kuongeza bajeti ya vifaa hivi ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika afya ya uzazi.

Kulingana na Nelly Munyasia wa Reproductive Health Network Kenya, mgogoro huu umeathiri huduma kwa wateja 6.2 milioni kila mwaka.

“Serikali inadai kuwa vifaa vilivyoko vitadumu kwa miezi mitano, lakini tunajua baadhi ya dawa tayari zimeisha,” alisema.

Waziri wa Afya, Debra Mulongo Barasa, alisema kuwa usitishaji wa ufadhili wa Amerika umeathiri huduma muhimu kama chanjo na matibabu ya Ukimwi.

Alisema kuwa Hazina ya Taifa inapaswa kutoa fedha za dharura kuzuia athari zaidi.

Kwa mujibu wa utafiti wa Hali ya Afya Kenya 2022, asilimia 14 ya wanawake walioolewa wenye umri wa miaka 15-49 wanahitaji mpango wa uzazi lakini hawawezi kupata huduma hizo, jambo linaloongeza hatari ya mimba zisizotarajiwa.