Waititu kuendelea kula maharagwe jela jaribio la pili la dhamana likipingwa
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu Baba Yao, atasalia gerezani kwa muda mrefu zaidi kabla ya Mahakama Kuu kuamua ikiwa itamwachilia kwa dhamana au la.
Hii inafuatia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, kupinga jaribio la Waititu na wenzake wawili kurekebisha rufaa yao na kuwasilisha upya maombi ya dhamana.
Waititu alishindwa katika ombi lake la awali la kuachiliwa kwa dhamana akisubiri rufaa yake kusikilizwa.
Jaji Lucy Njuguna alikataa ombi hilo, akisema kuwa sababu alizotoa hazikufikia viwango vya kisheria vinavyohitajika aachiliwe kwa dhamana.
Badala yake, jaji aliamuru kuwa Waititu aendelee na rufaa kuu ya kupinga kifungo cha miaka 12 alichohukumiwa.
Waititu alihukumiwa Februari 14 na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Ufisadi, Thomas Nzioki, kwa makosa ya ufisadi alipokuwa Gavana wa Kiambu.
Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/waititu-asotea-jela/
Mahakama ilimpata na hatia ya kupokea kwa njia haramu Sh25 milioni kutoka kwa kampuni ya Enterprise Testimony Limited, ambayo ilikuwa imeshinda zabuni ya ujenzi wa barabara ya thamani ya Sh588 milioni katika Kaunti ya Kiambu wakati wa uongozi wake.
Pia, alihukumiwa kwa kupokea fedha kupitia kampuni zake mbili akijua kuwa zilikuwa mali ya uhalifu.
Katika ombi lake la awali la dhamana, Waititu alidai kuwa anahitaji matibabu, lakini Jaji Njuguna alikataa ombi hilo, akisema kuwa huduma za afya katika magereza zinaweza kushughulikia matatizo yake ya kiafya.
Baada ya kushindwa mara ya kwanza, Waititu sasa amewaajiri mawakili mashuhuri akiwemo Wakili Mkuu Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Kibe Mungai, Ndegwa Njiru, na Wilfred Nyamu, ili kushinikiza kuachiliwa kwake kwa dhamana akisubiri rufaa yake kusikilizwa.
Hata hivyo, DPP amepinga vikali jaribio jipya la Waititu la kupewa dhamana, akisema kuwa suala hilo tayari limeshaamuliwa.
Kufuatia pingamizi hilo, Jaji Njuguna ameagiza pande zote kuwasilisha maelezo yao kwa maandishi kabla ya kutoa uamuzi mnamo Aprili 23.