Habari za Kaunti

Nyaribo: Nyamira ni kaunti yenye mabunge mawili, maspika na makarani wawili

Na MARY WANGARI March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Nyamira imegawanyika vibaya huku ikiwa na mabunge mawili ya kaunti, maspika wawili na makarani wawili wa kaunti hali inayowakosesha wakazi eneo hilo manufaa ya ugatuzi, Seneti imefahamishwa

Gavana Amos Nyaribo alieleza Kamati ya Seneti kuwa anatafakari kuwasilisha ombi kwa Rais William Ruto kuteua kamati maalum kuisimamia au hata kuivunjilia mbali kaunti hiyo.

Mkuu huyo wa kaunti alifika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Hesabu za Fedha za Serikali (CPAC) kujibu maswali kuhusiana na Sh5.8 bilioni za kaunti katika bajeti ya 2023/2024, suala ambalo halikufanyika kwa sababu ripoti ilichelewa kuwasilishwa.

Gavana aliyelazimika kusubiri kwa karibu saa tano kabla ya kukutana na Kamati inayoongozwa na Seneta wa Homabay Moses Kajwang, alistaajabisha maseneta alipokiri hakumjua karani wa kaunti hadi wiki iliyopita korti ilipotoa uamuzi.

Akifafanua sababu ya kuchelewesha majibu, Gavana Nyaribo alifichua mivutano ya uongozi inayokumba Nyamira akisema alipokea mialiko kutoka kwa makarani wawili mmoja wao akiwa “haramu” kwa sababu alitimuliwa afisini.

“Kwa kweli tumegawanyika sana. Hadi wiki iliyopita, korti ilipoamua ni nani karani anayefaa. Ni wajibu wangu kufuata uamuzi wa mahakama. Karani aliyekuwa akituma mwaliko alifurushwa lakini akaendelea kuituma,” Gavana Nyaribo alieleza.

Maseneta walichanganyikiwa zaidi ilipoibuka serikali ya Nyamira inaongozwa na kambi mbili kwa wakati mmoja ikiwemo katika bunge la kaunti, makarani wawili na maspika wawili.

Kulingana na Gavana, Nyamira ina Bunge mashinani linaloongozwa na Spika Enock Okero ambaye, kulingana na Bw Nyaribo, alirejeshwa na korti baada ya kutimuliwa, na bunge la pili linaloongozwa na spika “aliyetangazwa kuwa haramu.”

“Tumechanganyikiwa sana. Tunataka mtu atakayeweza kutuchorea taswira kamili ya kinachoendelea Nyamira. Yamkini kuna maspika wawili, makarani wawili, au hata magavana wawili, nani anayejua,” alisema mwenyekiti wa CPAC, Seneta Kajwang.

“Tulikuja kusaka majibu kuhusu zilivyotumika Sh5.8 bilioni lakini tumejipata tukifafanuliwa na gavana kuhusu yanayoendelea katika kaunti jambo ambalo ni la ajabu sana.”

Wakili wa kaunti ya Nyamira, Erastus Menge, alikiri kaunti hiyo imeandamwa na vita vikali kortini kuhusu ni nani aliye Spika halali kati ya Bw Okero aliyepatiwa kibali cha mahakama baada ya kung’atuliwa afisini, na diwani wa zamani katika Wadi ya Elerenyo, Thaddeus Nyabaro, aliyechaguliwa kama spika mpya Desemba 2024.

Kikao hicho kiligeuka jukwaa la majibizano na kurushiana lawama baina ya Gavana Nyaribo, Seneta wa Nyamira Erick Okong’o na madiwani.

Madiwani walimshutumu Gavana kwa kuanzisha bunge tofauti la kaunti na kuendesha shughuli muhimu za kaunti ikiwemo kupitisha bajeti na kuwapiga msasa maafisa wa kaunti ilhali kuna bunge rasmi la Nyamira.

Maseneta akiwemo Seneta wa Kitui, Enock Wambua, waliwarai viongozi wa Nyamira kuweka kando tofauti zao na kutafuta namna ya kufanya kazi pamoja la sivyo Seneti italazimika kuingilia kati kisheria.

Akijitetea, Gavana Nyaribo alisema Bunge Mashinani linaongozwa na Spika halali na kwamba vikao vyote vilichapishwa kwenye notisi rasmi.

Alisema ameitisha kikao wiki ijayo na madiwani waliochaguliwa kusuluhisha hali huku akimlaumu Seneta Okong’o na baadhi ya madiwani kwa kuchochea uhasama wa kisiasa Nyamira.

“Seneta wetu ndiye anayepuulizia moto na yuko hapa akionekana kama kasisi,” alisema Gavana.