Mwana Tik Toker Rish Kamunge mashakani kwa kashfa ya utapeli wa ajira
AJENTI wa kutafutia watu kazi ughaibuni ameona cha mtema kuni alipokamatwa na wananchi baada ya kujificha miezi miwili na mamilioni ya pesa akidai ni za kuwatafutia ajira ng’ambo.
Bi Maria Wangari Kamunge almaarufu Rish Kamunge, gwiji wa mtandao wa Tik Tok alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina baada ya kukamatwa na baadhi ya wananchi aliowatapeli.
Rish alipelekwa unyounyo Machi 26, 2025 hadi kituo cha polisi cha Central na kuzuiliwa, huku mamia ya watafuta kazi waliotapeliwa wakiandikisha taarifa kwa polisi.
Rish alikuwa ameandikisha kampuni kwa jina Trustpin Verified Agent Limited aliyodai ni ya kuwaunganisha wanaotafuta kazi na kampuni za mataifa ya ughaibuni zinazoajiri watu wa taaluma mbalimbali.
Kiongozi wa mashtaka Hillary Isiako aliomba Rish azuiliwe kwa siku saba kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi na kupata rekodi za M-Pesa kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.

Bw Isiako alieleza hakimu mshukiwa huyu wa utapeli amekuwa akisakwa na polisi baada ya ripoti kwamba amewapunja wananchi katika kashfa ya ajira.
Rish, hakimu alielezwa atatoroka iwapo ataachiliwa kwa dhamana.
Mahakama ilielezwa, “ikiwa alipokea kitita cha mimilioni ya pesa kutoka kwa watafuta kazi na kutoroka, akiachiliwa kwa dhamana atatoweka kabisa.”
Lakini wakili Lewis Gicheha aliyemwakilisha Rish alipuuzilia mbali madai ya DPP akisema hakuna mahali mshukiwa huyo ataenda.
Alisema uchunguzi ambao polisi wanafanya unaweza kuendelea kama mshukiwa yuko nje kwa dhamana.
Rish aliyefikishwa kortini saa 10 alasiri aliagizwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capiol Hill hadi Machi 28, 2025 korti itakapotoa uamuzi endapo ataachiliwa kwa dhamana au la.
Mahakama ilielezwa Rish alikuwa anapokea kati ya Sh200, 000 na Sh300, 000 kutoka kwa walalamishi kuwafanikishia haja yao ya kusaka kazi ng’ambo.