Habari za Kitaifa

Urais 2027: Maraga akana madai yeye ni mradi wa Serikali

Na WYCLIFFE NYABERI March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu mstaafu David Maraga amekanusha madai kwamba yeye ni ‘mradi’ unaofadhiliwa na serikali, akisema hilo litabainika bayana kadri muda wa uchaguzi mkuu wa 2027 unavyozidi kukaribia.

Bw Maraga, ambaye anatoka katika jamii ya Abagusii anasemekana kuwa na nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu 2027.

Jamii hiyo pia inajiandaa kumuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i katika kinyang’anyiro hicho.

Kutokana na hilo, wafuasi wengi wa Dkt Matiang’i, wamekuwa wakidai kuwa mienendo ya hivi karibuni ya afisa huyo wa zamani wa mahakama ni njama fiche iliyopangwa na serikali ya Kenya Kwanza kugawanya kura chache za Abagusii.

Lakini akizungumza Jumapili, Machi 30, 2025 baada ya kuabudu katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Kisii Mjini, Bw Maraga alipuuzilia mbali madai hayo na kuongeza kuwa ni Wakenya pekee watakaoamua ni kina nani watakuwa viongozi wao.

“Tukieni tu. Kwa wakati ufaao, mtajiamulia ikiwa mimi ni mradi wa serikali au la,” Bw Maraga aliwaambia waandishi wa habari nje ya majengo ya kanisa hilo.

Jaji Mkuu huyo mstaafu alisema ikiwa mtu angemuuliza, ni nani mgombea bora wa kuiongoza nchi mbele, angemwambia mtu huyo kuwa yeye ndiye.

“Ukiniuliza, nitakuambia mimi ndiye sahihi na wengine pia watakuambia kuwa wao ndio bora. Mwisho wake, ni watu wa Kenya ambao watafanya uchaguzi,” Bw Maraga alisema.

Bw Maraga, hata hivyo, alikwepa maswali mengi ya wanahabari akisema kwamba hakutaka kutoa maoni zaidi katika mazingira hayo kwa sababu kufanya hivyo kutaonekana kama njia moja ya kupinga makanisa, ambayo yamekuwa yakiwakemea sana wanasiasa kwa kuiteka nyara ili kuendeleza ajenda zao za kisiasa.

Kuhusu mchakato unaoendelea wa kubuni upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Maraga alisema kuwa anatumai kuwa zoezi hilo la kuchagua mwenyekiti wa tume na makamishna wake litakuwa wazi na la kuteua watu wenye uadilifu kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

“Tunaomba wachague watu wema, watu waaminifu ili kutoa uchaguzi huru na wa haki,”Bw Maraga aliongeza.

Tangu Ijumaa, Bw Maraga amekuwa akipiga kambi katika Kaunti za Migori na Kisii, akikutana na Wakenya na wadau wengine.

Siku ya Ijumaa, Bw Maraga alikuwa mzungumzaji mkuu katika hotuba ya umma katika Chuo Kikuu cha Rongo.

Mhadhara huo ulizingatia nguzo za kisiasa za utawala, umuhimu wa Katiba na utawala wa sheria katika kuunda jamii yenye haki.

Juzi, Bw Maraga alijiunga na waumini wa dhehebu lake la Waadventista Wasabato (SDA) katika Kaunti ya Migori kabla ya kuvuka hadi Kisii Jumapili.