Mswada bungeni kuharamisha uvutaji sigara kwa wenye miaka chini ya 100
AFP Na PETER MBURU
MBUNGE mmoja kutoka jimbo la Hawaii nchini Marekani amefikisha mswada bungeni ambao unalenga kuharamisha matumizi ya sigara kwa watu wa umri chini ya miaka 100.
Mbunge huyo wa chama cha Democratic Richard Creagan anapendekeza sheria, ambayo huenda ikawa kuharamishwa kwa sigara kabisa kufikia mwaka 2024.
Tayari sasa Hawaii ina sheria kali zaidi zinazopinga uvutaji sigara, lakini Creagan ambaye ni daktari bado anaamini kuwa hatua zaidi zinahitaji kuchukuliwa kuzuia matumizi yake, akitaja dawa hiyo kuwa hatari zaidi mwilini mwa binadamu.
Katika sheria ya sasa, sharti mtu awe na miaka 21 ili aruhusiwe kununua sigara Hawaii, huku taifa zima umri huo ukiwa kuanzia miaka 18 au 19.
Lakini sasa mswada wa Creagan unapendekeza umri wa mtu kuruhusiwa kununua sigara upandishwe hadi miaka 30 kufikia mwaka ujao, miaka 40 mnamo 2021, miaka 50 mnamo 2022 na miaka 60 mnamo 2023.
Kufikia mnamo 2024, mbunge huyo anapendekeza umri wa watu wanaoruhusiwa kununua ama kutumia sigara uwe miaka 100.
“Serikali ina jukumu la kulinda afya ya umma,” akasema Creagan, ambaye alisema kuwa pia naye alivuta sigara wakati alipokuwa akisomea masomo ya udaktari.
Alilaumu kampuni za kutengeneza sigara kuwa zimewafanya watumizi fulani kuwa watumwa wa dawa hiyo, mbali na kuharibu afya yao.
Kulingana na kituo cha udhibiti na uzuiaji wa magonjwa, uvutaji sigara ndio kiini kikuu cha magonjwa yanayoweza kukingika na vifo nchini Marekani, ukichangia vifo vya watu nusu milioni kila mwaka.