Kimataifa

Sababu ya wanaume kuzeeka mapema kuliko wanawake

February 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

AFP Na PETER MBURU

UTAFITI mpya umedhihirisha sababu ya wanawake kuishi maisha marefu kushinda wanaume na akili zao kuwa imara hadi uzeeni, ukisema akili za wanawake kwa kawaida huwa changa kwa miaka mitatu, zaidi ya za wanaume.

Utafiti huo ulifanyiwa wanawake 121 na wanaume 84, wote ambao walipimwa akili, namna hewa inazunguka akilini mwao na kiwango cha Glucose akilini.

Waliofanyiwa utafiti walikuwa wa kati ya miaka 20 na 80 na akili za wanawake zilibainika kuwa na uchanga ikilinganishwa na za wanaume kwa kuzingatia namna zinatumia na kusambaza madini ya sukari na Glucose.

Hii ni kwa kuwa kama sehemu zingine za mwili, akili pia hutumia madini ya sukari kupata nguvu (ya kufanya kazi) na namna akili inasambaza madini ya Glucose inaweza kueleza kuhusu uzee wake.

Utafiti huu ulifanywa na taasisi ya National Academy of Sciences ya Marekani.

Ulionyesha kuwa akili za wanawake kwa kawaida huwa na udogo wa miaka 3.8 ikilinganishwa na umri wao wa kweli. Za wanaume nazo zilionekana kuwa na udogo wa miaka 2.4, ikilinganishwa na umri wao wa kweli.

“Si kuwa akili za wanaume huzeeka kwa haraka. Wanaanza kufika utu uzima miaka mitatu kabla ya wanawake na hilo linaendelea maisha yote,” akasema Manu Goyal, Profesa msaidizi katika chuo kikuu cha Washington, idara ya matibabu.

Wazo moja ambalo linaweza kueleza matukio haya linadhaniwa kuwa mabadiliko ya homini, ambayo huenda huadhiri matukio ya kukua kwa mwili kuanzia umri mdogo na kuwafanya wanawake kuwa wachanga maisha yote.

“Inawezekana kuwa sababu wanawake hawashuhudii kuzeeka kwa akili na kudorora kwa mawazo miaka ya uzeeni ni kwa kuwa akili zao husalia change hadi maisha yote,” akasema Goyal.

Kazi zaidi inazidi kufanyiwa utafiti huo ili kubaini na kuelewa athari ama mambo mengine ambayo unaweza kudokeza.