Daktari wa makalio aliyesababisha kifo cha mteja arushwa ndani
DAKTARI wa masuala ya urembo anayeshtakiwa kumuua mwanamke aliyemfanyia upasuaji kumjengea makalio manene amenyimwa dhamana na Mahakama ya Kibra.
Hakimu mwandamizi Bw Samson Temu aliamuru Dkt Robert Maweu Mutula pamoja na wamiliki wa Hospitali ya Omnicare Medical Limited almaarufu Body By Design (BBD) George Wakaria Njoroge na muuguzi Lilian Edna Wanjiru Mwariri wasalie rumande hadi Aprili 15, 2025 ripoti ya urekebishaji tabia iwasilishwe mahakamani.
Bw Temu aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mumewe Lucy Wambui Kananu, watoto wake pamoja na familia za washtakiwa kabla ya kuamua ikiwa washtakiwa wataachiliwa kwa dhamana.
“Kiongozi wa mashtaka na mawakili wanaowakilisha washtakiwa wamezingatia tu haki za washukiwa na wala hawakujali haki za wahasiriwa,” Bw Temu alisema.
Hakimu alisema dhamana ni haki ya washtakiwa.
Pia, alisema lazima mahakama itilie maanani haki za wahahasiriwa ambao walimpoteza mtoto, mke, mama kabla ya kuamua ikiwa washtakiwa watapewa dhamana.
Bw Temu aliamuru washtakiwa wasalie rumande hadi Aprili ripoti ya washtakiwa itakapowasilishwa kortini.
“Ni baada ya kupokea ripoti ya wahasiriwa hii korti itakazingatia mawasilisho ya washtakiwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuhusu dhamana,” alisema hakimu.
Dkt Mutula, Njoroge na Wanjiru walikanusha Jumatano shtaka la kumuua bila ya kukusudia Lucy Wambui Kamau Oktoba 16, 2024.
Mawakili Danstan Omari, Cliff Ombeta, Samson Nyaberi na Shadrack Wambui wanaowakilisha washtakiwa walieleza mahakama kwamba Daktari huyo ameshtakiwa kimakosa na shtaka alilofunguliwa halina mashiko kisheria.
“Kumshtaki Dkt Mutula kwa mauaji ni makosa makubwa kwa vile hakuwa na nia ya kumuua Wambui alipomhudumia kiafya,” Bw Omari alieleza mahakama.
Alisema hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kumshtaki Dkt Mutula ni tisho kwa kila taaluma.
“Watalaamu wa kazi wanakondolewa na hatari ya kushtakiwa makosa yanapotokea. Dkt Mutula hakuwa na nia ya kuua alipomhudumia Wambui Oktoba 16, 2024,” Bw Omari alisema.
Alieleza mahakama kwamba endapo kuna makosa yalitokea, basi baraza la madaktari na wenye maduka ya kuuza dawa (KMPDC) ndilo lingeshughulikia suala hilo.
Bw Omari alisema baraza la KMPDC halikuchunguza madai kwamba Dkt Mutula alikosea.
“Nimewasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga hatua ya DPP kuamuru Dkt Mutula, Njoroge na Wanjiru washtakiwe kwa mauaji ilhali KMPDC haijapewa fursa ya kushughulikia suala hili,” alisema Bw Omari.
Katika mukhtadha huo, aliomba washtakiwa waachiliwe kwa dhamana huku upande wa mashtaka ukipinga ombi hilo.
Mutula, Njoroge, Mwairi na Omnicare iliyoko kwenye barabara ya Kabasiran, Nairobi wanakabiliwa na shtaka la kuua bila kukusudia kinyume na sheria nambari 202 kama inavyosomwa, sambamba na kifungu 205 cha sheria za jinai.
Katika kesi aliyoshtaki mahakama kuu, Omari ameomba DPP azimwe kuwashtaki Dkt Mutula na wenzake kwa mauaji na badala yake kesi hiyo ipelekwe kwa bodi ya KMPDC kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria
“Naomba hii mahakama iwaachilie washtakiwa kwa dhamana tukisubiri uamuzi wa mahakama kuu iwapo kesi hii itapelekwa kuamuliwa na bodi ya KMPDC,” Bw Omari alimsihi Bw Temu.
Katika kesi iliyoko mbele ya Jaji Diana Kavedza, Dkt Mutula amedokeza kwamba marehemu alienda katika hospitali ya Omnicare Oktoba 16, 2025 na kufanyiwa utaratibu unaojulikana kiutalaamu – Liposuction.
Baada ya kushughulikiwa, marehemu aliruhusiwa kwenda nyumbani.
Wambui alienda katika hospitali nyingine ambapo alifia na wala hakuaga akiwa Omnicare.