Habari za Kitaifa

Ruto: Habari feki mitandaoni ni tishio kwa usalama wa taifa  

Na  KENNEDY KIMANTHI April 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameonya kwamba habari feki zinaendelea kuwa tishio kwa usalama wa kitaifa huku maafisa wa usalama wakisema imekuwa vigumu kwa serikali kudumisha usalama kutokana na mienendo ya watu kutumia mitandao ya kijamii kupanga machafuko.

Rais alisema mienendo ya uenezaji habari za kupotosha kupitia mitandao ya kijamii ni tishio kwa usalama wa nchi.

“Habari za uwongo, madai ya kupotosha na kuvurugwa kwa ukweli huharibu taarifa zinazotolewa kwa umma na kuvuruga taasisi za kidemokrasia. Majukwaa ya mitandao ya kijamii yanapotumiwa kueneza chuki, uchochezi, itikadi kali husababisha kukithiri kwa utovu wa usalama,” akasema.

Ili kukabiliana na janga hili la kidijitali, Rais Ruto alisema serikali inatekeleza mikakati mbalimbali, inayolinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata habari sahihi,” akasema.

Alikuwa akiongea Ijumaa, Aprili 4, 2025 katika Kongamano la Pili la Ushirikiano wa Mashariki, mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru ambapo masuala yanayohusu hatari ya matumizi ya mitandao ya kijamii yalijadiliwa.

Kando na katika jukwaa la kidijitali, Rais alisema, sawa na nchi zingine za ulimwengu, Kenya inakabiliwa na aina za kawaida za tishio ya usalama.

“Uwepo wa hatari katika mataifa mbalimbali unahitaji kukabiliwa katika njia shirikishi na inayoongozwa na utoaji habari za kijasusi. Nafurahi kuwa maudhui ya mwaka huu yanaakisi changamoto za nyakati hizi. Kwa hivyo, tunapaswa kuchukua hatua ili kudumisha amani kikanda na kimataifa,” Rais Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alizitaka asasi za ujasusi, watungaji sera na wadau katika sekta ya utoaji misaada ya kibinadamu kuanza kuchukulia mabadiliko ya tabia nchini kama tishio la usalama wa kitaifa.

Mnamo Alhamisi, Aprili 3, 2025 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Noordin Haji alionya kuwa majukwaa ya kidijitali yanatumiwa kupotosha na kuchochea fujo Barani Afrika.

“Hali hii imechangia kuibuka kwa usambazaji wa habari za kupotosha raia, na kupelekea wao kuwa na dhana potovu kuhusu serikali zao,” akasema.

Kauli ya Haji ilijiri miezi kadhaa baada ya wimbi la maandamano ya mwaka jana, 2024, ya vijana ya kizazi cha Gen Z kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Maandamano hayo, ambayo yalipangwa na kushirikishwa kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii, yalishuhudiwa katika kaunti 36 nchini.

Zaidi ya watu 70 waliuawa katika maandamano hayo huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

Maandamano hayo yalionyesha jinsi majukwaa ya kidijitali yamegeuka kuwa vyombo muhimu vya umma kubadilishana mawazo na hata kupanga fujo.

Katika miezi ya hivi karibuni, visa vya utekaji nyara na mauaji ya vijana wanaotumia majukwaa hayo kuchochea chuki dhidi ya serikali vilisheheni mitandaoni.

Wiki jana, Bw Haji pia alionya kuwa mashindano ya kisiasa hayafai kuleta misukosuko nchini, akitaka umma kujiepusha na siasa za migawanyiko.