Habari za Kitaifa

Mnada wa ajira serikalini barua zikiuziwa wenye pesa

Na BRIAN WASUNA April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Mfumo wa ajira serikalini nchini Kenya unazidi kugubikwa na ufisadi ambapo nafasi zimegeuka kuwa bidhaa sokoni, zikiuzwa kwa walio na pesa au uhusiano wa kisiasa.

Gerald Kung’u Wamaitha, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 2015, alikatiza ndoto yake ya kufundisha baada ya kuombwa Sh100,000 kama hongo ili kupata ajira kutoka Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Wakati huo huo, wabunge 11 wanaohusishwa na serikali ya Kenya Kwanza walisemekana kupewa kila mmoja nafasi 20 za ajira za walimu kwa wapiga kura wao.

Hili lilidhihirika baada ya mwakilishi wa kike wa Murang’a Betty Njeri Maina kufichua hadharani namna siasa zinavyoingilia ajira ya walimu. Mwezi Mei 2024, aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitoa barua ya TSC katika mazishi, huku wengine kama Mbunge Sylvanus Osoro wakidai walipokea hadi barua 100 za TSC.

Katika jeshi, aliyekuwa mwanajeshi Fred Kiptum Kiplagat alihukumiwa kifungo cha miaka 5.5 kwa kupokea Sh300,000 kutoka kwa kijana mmoja ili kumsaidia kujiunga na KDF. Mwingine, Ruben Ngige Muthoni, alijitokeza kuelezea jinsi alivyoshiriki usajili wa makurutu wa KDF, akachukuliwa alama za vidole na kupewa barua ya kuripoti, lakini hadi leo hajaitwa wala kurejeshewa kitambulisho chake.

Katika Polisi, ripoti ya Tume ya Maraga ya 2023 ilifichua kuwa baadhi ya maafisa wa juu walikuwa wakitoa nafasi za ajira kwa hadi Sh600,000. Nafasi nyingi za kupandishwa vyeo zimekuwa zikitolewa kwa marafiki, familia za wanasiasa, au wale walioweza kutoa hongo.

Uozo huu umeenea hata katika mashirika mengine ya serikali kama Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA), ambapo mwaka 2014 Jaji William Musyoka alifuta ajira za watu 1,406 baada ya kugundua kuwa asilimia 56 ya nafasi hizo zilienda kwa jamii mbili pekee — Kikuyu na Kalenjin.

Wakenya wengi, hasa vijana waliohitimu, wanaendelea kunyimwa nafasi za ajira licha ya kustahiki, kwa sababu ya mfumo wa mnada unaowapa nafasi wale walio na hela au uhusiano wa karibu na wenye mamlaka.