Habari za Kitaifa

Mudavadi akanusha kwamba ameunda chama kipya, asisitiza yuko UDA

Na BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, amepuuzilia mbali madai kwamba ameunda chama kipya cha kisiasa miezi michache baada ya kuvunja chama chake cha Amani National Congress (ANC) na kujiunga na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake ya mawasiliano jana Aprili 6, Mudavadi alieleza wazi kuwa bado yuko ndani ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

‘Mheshimiwa Musalia Mudavadi, Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Wakenya wanaoishi ng’ambo, anaeleza kusikitishwa na ripoti katika baadhi ya vyombo vya habari zinazomhusisha na chama kipya cha kisiasa,’ ilisoma taarifa hiyo iliyotiwa saini na Jacob Ngetich.

‘Kwa kuondoa mashaka yoyote, Bw Mudavadi yuko imara ndani ya serikali ya muungano wa Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.’

Taarifa hiyo pia ilisisitiza kwamba chama cha ANC kiliingia katika muungano wa Kenya Kwanza kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 pamoja na vyama vingine, na baadaye kikavunjwa rasmi na kumezwa na UDA mnamo Januari 17.

Aidha, ofisi ya Mudavadi ilibainisha kuwa ameendelea kuwa mtu wa uadilifu, mkweli na mwenye heshima katika mienendo yake ya kisiasa, na hajawahi kuwa na ujanja wowote.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa uamuzi wake wa kuungana na UDA haukuwa wa kulazimishwa bali ulikuwa wa hiari na uliidhinishwa na wanachama wa chama hicho.

Hili linadhihirika kupitia nafasi za juu walizopata maafisa wa zamani wa chama cha ANC, ikiwemo Kaimu Kiongozi wa zamani wa chama, Issa Timamy, ambaye alihifadhi nafasi yake ndani ya UDA.

‘Mudavadi anaendelea kutekeleza majukumu yake ya serikali kwa bidii katika kuwahudumia Wakenya, na hana nia yoyote ya kujiunga na chama kingine cha kisiasa,’ ilisema taarifa hiyo