Habari za Kitaifa

IEBC: Maswali yaibuka majina 6 yakipenyezwa kichinichini kuhojiwa

Na DAVID MWERE na CHARLE WASONGA April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASWALI yameanza kuibuka kuhusu uadilifu na uhalali wa mchakato unaoendelea wa uajiri wa Mwenyekiti na Makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hii ni baada ya kuibuka kuwa majina ya watu sita yalipenyezwa kwenye orodha ya watu 105 wanaosailiwa kujaza nafasi sita za makamishna wa tume hiyo.

Watu hao sita ambao kujumuishwa kwao kwenye orodha hiyo kumeibua maswali, ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa mkoa Bw Hassan Noor Hassan, Jibril Maalim Mohamed, ⁠Michael Ben Oliewo, ⁠ Charles Kipyegon Mutai, ⁠Stephen Kibet Ngeno na ⁠Joel Mwita Daniel.

Majina ya sita hao hayakuwa kwenye orodha ya awali ya watu 105, ambayo ilichapishwa rasmi magazetini, japo waliwasilisha maombi.

Ufichuzi huo umejiri siku chache baada ya Bunge la Kitaifa kuliongezea jopo linaloendesha shughuli hiyo muda wa siku 14 zaidi, bila sababu maalum.

Hii ni baada wa wabunge wa mirengo yote miwili mnamo Aprili 2, kupitisha hoja iliyodhaminiwa na Kiranja wa Wachache Junet Mohamed.

Kufuatia hatua hiyo jopo hilo linaloongozwa na Nelson Makanda, sasa litatarajiwa kukamilisha shughuli hiyo, na kuwasilisha ripoti yake bungeni, kabla au mnamo Mei 12, badala ya Aprili 28, 2025.

Na mnamo Aprili 1, ukungu mwingine uligubika shughuli hiyo baada ya viongozi wa upinzani kudai kuna njama ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuidhibiti kwa manufaa yao.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua, na Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, walidai Rais Ruto na Bw Odinga wanalenga kuhakikisha kwamba ni watu waaminifu kwao pekee watakaoteuliwa kwa nafasi hizo muhimu.

Hili kwa mujibu wa viongozi hao litatoa mwanya wa wizi wa kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tunashangazwa na jinsi utawala wa Ruto umejizatiti kudhibiti na kuelekeza mchakato wa uajiri wa makamishna wa IEBC kwa lengo la kuteka asasi hiyo itakayosimamia uchaguzi.

“Huu ni mpango mchafu, ambao tunaamini unalenga kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao ili kuendeleza utawala wa Kenya Kwanza ambao tayari umepoteza imani ya Wakenya,” alisema Bw Musyoka kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Serena.

Wanasiasa hao walipinga kuorodheshwa kwa aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Charles Nyachae na Mwenyekiti wa Kampuni ya Umeme Nchini (KPLC), Joy Mdivo, miongoni mwa watakaoshindania nafasi ya mwenyekiti wakidai ni washirika wa Rais Ruto.

Kuhusu kujumuishwa kwa watu sita wapya kwenye orodha ya wanaosailiwa wakati huu, wanasheria wanasema hiyo ni kinyume cha Sheria ya IEBC ya 2024 iliyobuni jopo la wanachama tisa kuajiri mwenyekiti na makamishna wa tume hiyo.

Wanaonya kuwa hatua hiyo inatilia shaka uadilifu wa mchakato huo na inaweza kuchangia kuwasilishwa kwa kesi kortini kuharamisha shughuli hiyo wakati huu “ambapo taifa linahitaji makamishna wapya wa IEBC kwa dharura.”

Bw Bobby Mkangi, ambaye ni mmoja wa wataalamu wa masuala ya kikatiba walioandika Katiba ya sasa, anasema maelezo kamili yanapasa kutolewa kuhusu mantiki ya kujumuishwa kwa majina hayo sita “ambayo hayakuwa kwenye orodha halisi.”

“Hili si jambo la kawaida, ni haramu, linakiuka maadili na zaidi ya hayo ni kinyume cha Katiba,” akaeleza.

“Hatua hii inatilia shaka uadilifu na uhalali wa shughuli hii ya usaili wa makamishna wa IEBC,” Bw Mkangi akaongeza.

Kasisi Makanda hakujibu maswali yetu, tuliyotuma kupitia nambari yake inayojulikana, tulipotaka kujua sababu iliyochangia kujumuishwa kwa majina ya watu hao sita kwenye orodha ya wanaofanyiwa usaili wakati huu.