Habari za Kitaifa

Raia Mhindi azuiwa kuenda India kupata matibabu akikabiliwa na kesi ya wizi wa mamilioni

Na RICHARD MUNGUTI April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MCHAPISHAJI na mwandishi maarufu wa vitabu Dhillon Malkiat Singh ameomba mahakama imwagize Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga afike kortini mwenyewe kutoa mwanga kuhusu wizi wa Sh254 milioni dhidi ya raia wa India Cheekati Naramshi Rao.

Malkiat aliyepinga Cheekati akiruhusiwa kusafiri kabla ya kesi inayomkabili kumalizika, aliomba DPP aamriwe afike kortini atoe udhamini kwamba mshtakiwa atarudi nchini akikubaliwa kusafiri.

Malkiat alisema Cheekati amejaribu kutoroka Kenya mara tatu, baada ya wizi huo na ughushi wa sahihi yake kugunduliwa.

Kupitia kwa wakili Kimani Wachira, Malkiat alimfichulia hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Carolyne Nyaguthii kwamba Cheekati amejaribu kutoroka mara tatu alipojua anachunguzwa na maafisa wa Idara ya Uhalifu na Jinai (DCI).

Lakini juhudi zake zilipigwa dafrau na hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina, ambapo alimwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji ahakikishe Cheekati hatatoka nchini.

Pia, Cheekati aliagizwa awasilishe pasipoti yake kortini.

Bw Kimani alieleza mahakama mshtakiwa anatumia mbinu ya kudai baba yake ni mgonjwa mahututi.

“Hii mahakama ikimkubalia mshtakiwa kusafiri, itakuwa ndiyo imemsaidia kutoroka,” Bw Kimani alieleza mahakama.

Korti ilielezwa kwamba mshtakiwa ameweka katika akaunti za ng’ambo kiwango kikubwa cha pesa, zikiwemo Sh254 milioni anazodaiwa aliiba kutoka kwa kampuni ya kupiga chapa.

Akiwasilisha ombi la kuruhusiwa asafiri, Cheekati alifichua baba yake mwenye umri wa miaka 80 ni mgonjwa na amemwagiza aende amwone kabla ya kuzidiwa na ugonjwa.

Isitoshe, alisema atatumia wakati huo kuona madaktari wake.

Lakini mahakama imeambiwa na Malkiat Singh kwamba mshtakiwa anatumia ugonjwa wa baba yake kama kisingizio na “anataka kutoroka.”

Hakimu alifahamishwa kuwa mshtakiwa aliingia nchini 2004 na hajakuwa akienda nyumbani.

“Mshtakiwa amekuwa hamtembelei baba yake. Watu wengine wa familia yake wamekuwa wakimtunza akiwa humu nchini Kenya,” Bw Kimani alieleza mahakama.

Bi Nyaguthii atatoa uamuzi wake mnamo Mei 5, 2025.

Cheekati amekanusha shtaka la wizi na kughushi wa sahihi ya Malkiat aliyotumia kujiandikia barua ya kupandishwa cheo kuwa Mkurugenzi wa kampuni ya kupiga chapa.