• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Mbegu mbovu zasababisha uhaba wa viazi nchini

Mbegu mbovu zasababisha uhaba wa viazi nchini

Na WACHIRA MWANGI

KENYA inakumbwa na uhaba wa tani 1.7 milioni za viazi kwa sababu ya wakulima wanatumia mbegu mbovu zisizotoa mazao mengi, Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri amesema.

Uhaba huo umefanya bei ya viazi izidi kupanda na kuwafanya wafanyabiashara kuagiza zao hilo kutoka mataifa ya nje.

Mbali na matumizi ya nyumbani, sekta ya hoteli nchini hutegemea pakubwa zao hilo kwa upishi wa aina mbalimbali za vyakula.

Waziri Kiunjuri alisema wakulima wanafaa watumie mbegu zilizoidhinishwa na serikali ili kuongeza mazao yao.

“Kwa mwaka mmoja ujao tutajaza pengo lililopo kwa kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu zinazofaa. Kufikia sasa, kiwango cha uzalishaji mbegu ni tani 6,700 ilhali kunahitajika tani 30,000,” akasema.

Alikuwa anahutubia kikao cha Kamati ya Bunge kilichofanyika mjini Mombasa.

Alisema kupitia njia hii, wakulima watafanikiwa kuvuna tani 10 za viazi kutoka kwa hekta moja ya shamba, ambayo ni sawa na magunia 88.

Waziri huyo aliongeza kuwa wakulima watakuwa wakitumia mbegu hizo mara tatu na hivyo basi kupunguza gharama ya kununua mbegu mara kwa mara.

Wakulima wa viazi wamekuwa wakilalamikia kupunjwa na wafanyabiashara hasa kuhusiana na jinsi ya kupima mazao yao.

“Suala kuu sasa ni kuhusu sheria zinazosimamia kilimo cha viazi. Kuna mambo mengi ambayo hayafanyiki jinsi inavyofaa na hii imesababisha kudhulumiwa kwa wakulima.”

Kuhusu suala la vyakula na virutubishi nchini, waziri alisema wizara yake itabuni mwongozo maalumu kuhakikisha Kenya inaweza kujitegemea kulisha wananchi wake.

You can share this post!

Murathe afichua kiini cha uhasama wake na Ruto

Kenya yapoteza watalii 2,000 wakihofia usalama

adminleo