Taharuki mbuzi wagonjwa wakifa kwa wingi, mizoga ikitupwa kiholela
WAKAZI wanaoishi eneo la Korompoi, kaunti ndogo ya Isinya, wamegubikwa na taharuki baada ya mbuzi waliowekwa karantini na idara ya kutibu mifugo eneo hilo kuzidi kufariki kwa wingi na mizoga yao kutupwa kiholela.
Katika kipindi cha wiki mbili, mbuzi wasiopungua 3,000 wamezuiliwa na mwekezaji wa kigeni kwenye kipande cha ardhi cha nusu ekari alichokodisha kwa miezi miwili.
Eneo hilo limedhibitiwa kumaanisha ufugaji ni marufuku. Inasemekana wanyama hao wanakufa kwa idadi kubwa kila siku.
Wakazi wamedai katika muda wa wiki mbili zilizopita eneo lote limegubikwa na uvundo wa mizoga inayodaiwa kutupwa kila pembe.
“Kila asubuhi, wanyama waliokufa hurundikwa pembeni mwa ardhi hiyo na wachungaji. Ni nadra kwa mizoga hiyo kuzikwa ipasavyo. Tumezoea uvundo unaohanikiza kutoka hapo,” alisema mwenyekiti wa Muungano wa Wakazi Korompoi (KOREA), Njeri Muriithi.
“Tunahofia kusambaa kwa maradhi ya wanyamamwitu. Genge la fisi wanarandaranda eneo hili usiku.”
Kwenye notisi ya karantini kwa siku saba iliyoonekana na Taifa Leo iliyotolewa na daktari wa mifugo Kajiado Mashariki, Topirian Kerempe, Aprili 2, 2025, wanyama hao waliwekwa karantini na kuzuiliwa kutembea hadi notisi nyingine itakapotolewa ili kuzuia kusambaa kwa maradhi.
Aidha, mmiliki wa wanyama hao aliagizwa kuzika mizoga kwenye shimo la fiti nne au kuiteketeza.
“Hakuna mnyama mwingine atahamishwa kutoka eneo lingine isipokuwa awe ametibiwa kwa namna iliyoelekezwa na Afisa wa kutibu mifugo au inspekta anayesimamia eneo hilo. Mizoga ya wanyama wote wanaokufa kutokana na ugonjwa huo kuanzia sasa itazikwa kwenye kimo kisichopungua futi nne chini ya ardhi au kuteketezwa kwa gharama ya wamiliki,” notisi ya karantini iliamuru.
Udadisi uliofanywa na Taifa Leo mnamo Jumanne, Aprili 8, 2025 uliashiria wanyama dhaifu waliosalia wakizunguka huru eneo hilo.
Mizoga ya mbuzi wapatao 50 waliokufa Jumatatu, Aprili 7 usiku haikuwa imeokotwa kutoka mazizi yao yanayolindwa vikali na kundi la wachungaji.
Majirani walielezea hofu kuwa nyama ya mizoga huenda ilipenyezwa kwenye maduka ya kuuzia nyama Kitengela na kuhatarisha maisha ya wanunuzi wasio na habari.