Ian Mbugua: Ni aibu kwa Ruto kuvuruga wanafunzi wa Butere Girls kuonyesha ugwiji wao katika usanii
WAIGIZAJI wamejitokeza kuichamba serikali ya William Ruto kufuatia varangati la kutumia nguvu ya polisi kuvuruga watoto wa shule ya upili kutoonyesha mchezo wao wa kuigiza wa ‘Echoes of War’.
Ni mchezo ambao umedaiwa kuingilia na kuukosoa vikali utawala wa Rais Ruto na hivyo kutokana na tamthilia hiyo, serikali iliamua kutumia nguvu za jeshi lake la polisi kuvuruga jambo ambalo lilifanya mada hiyo kutrendi.
Mwigizaji mkongwe Ian Mbugua akitoa kauli yake, ameikosoa serikali ya Ruto.
“Wanachokifanya sio haki, mbona wanaogopa si ni mchezo wa kuigiza tu. Kwa nini mtu anakwazwa, eti mchezo sio mzuri, kasema nani? Nani huyo ana tatizo na mchezo wenyewe kiasi cha kuufungia atuelimishe maana hatuelewi ubaya upo wapi?” amesema.
Mchekeshaji na mtengenezaji filamu Abel Mutua naye katoa makavu kwa serikali.
”Hii si aibu, yaani watoto wamemfanya mtu amepaniki kweli. Tamthilia kuna mtu serikalini kahisi inamwingilia na hajafurahia wakati hajatajwa. Yaani anapanikia kiasi cha kutumia fujo za polisi kuwavuruga watoto wadogo. Hii ni aibu.”