Habari za Kitaifa

Serikali kudhibiti idadi ya miradi kwa wanakandarasi kukabili uzembe

Na CECIL ODONGO April 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI inalenga kuanzisha sera ambayo itadhibiti idadi ya miradi ya serikali ambayo mwanakandarasi anaweza kupokezwa zabuni ya kuitekeleza ili kuhakikisha inakamilishwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Wafanyakazi Ikulu anayesimamia mipango na uwajibikaji, Bw Eliud Owalo, hatua hii inalenga kuhakikisha mwanakandarasi hachukui miradi mingi na kisha kushindwa kuitekeleza.

“Kama serikali, tunaenda kuibuka na sera ambayo itadhibiti idadi ya miradi ambayo mwanakandarasi anawania. Hii itazuia mwanakandarasi kuchukua miradi mingi kisha kulemewa kuikamilisha kwa wakati,” akasema Bw Owalo.

Aidha, serikali imetambua kuwa baadhi ya wanakandarasi baada ya kufaulu kupata zabuni ya miradi mbalimbali huzembea kumaliza kazi kwa wakati licha ya kupokea malipo yao.

Hali hii ndiyo husababisha serikali kulemewa kumaliza miradi iliyoahidi kwa wakati, hatua ambayo huvutia ghadhabu za raia na kusawiri utawala huu kama usiotimiza ahadi.

“Nawaonya wanakandarasi kuwa hatutaruhusu mwenendo huu wa kuzembea kutekeleza miradi uendelee. Kama mwanakandarasi amelipwa, lazima ahakikishe amekamilisha miradi kwa muda ambao umewekwa,” akaongeza.

Kuhakikisha kuwa wanakandarasi wanatii, wale ambao watachelewesha utekelezaji wa miradi ya serikali, watapigwa marufuku kukumbatia miradi mingine ya serikali.

Hatua hii itahakikisha kuna uwazi katika matumizi ya pesa za walipa ushuru na majukumu lengwa.

“Wanakandarasi wenye tabia hii watazimwa kutekeleza miradi mingine ya serikali kwa hivyo wao ndio sasa wana wajibu wa kuimarisha utendakazi wao,” akaongeza Bw Owalo.

Utawala wa Kenya Kwanza umekuwa ukikabiliwa na shutuma kutoka kwa raia kwa kutoa ahadi ya miradi ilhali miradi yenyewe huwa haikumbatiwi na ile iliyoanzishwa haikamilishwi kwa wakati.

“Kama serikali, tuna wajibu na uwajibikaji kwa umma na tukishafanya kazi yetu ya kumpa kazi mwanakandarasi, ni lazima afuate yaliyomo kwenye mkataba wake. Hatutaruhusu mwanakandarasi achukue miradi mingi kisha alemewe ilhali pesa ashapokea kutoka kwa serikali,” akasema waziri huyo wa zamani wa teknolojia na mawasiliano (ICT).