Habari

Sitaacha kuongea na Gachagua, asema Moha Jicho Pevu akimtaka Rais atatue zogo UDA

Na WINNIE ATIENO April 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Nyali Mohammed Ali amepasua mbarika na kumsihi Rais William Ruto kuingilia mgogoro katika chama tawala cha UDA akisema kuna malumbano makubwa.

Bw Ali ambaye aliingia bunge kwa muhula wa kwanza baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2017 kama mgombea huru, alisema haogopi lolote wala yeyote akiwataka wanasiasa kuwa waaminifu kwa umma badala ya kuabudu viongozi.

Bw Ali ambaye alikuwa pia mwanahabari wa ujasusi kwa zaidi ya mwongo alisema hatokubali kukandamizwa kwenye ulingo wa siasa.

“Nilishinda uchaguzi mkuu wa 2017 kwa kura 26,000 kama mgombea huru na kuangusha wanasiasa ambao walimwaga pesa lakini wapiga kura walinichagua mimi. Nilikuwa nimetoka ODM na kunyimwa tikiti. Mwaka wa 2022 niliunga chama cha UDA na kukipigia debe hata kuweka maisha yangu kwenye hatari na nikaibuka mshindi wa kiti cha Nyali na kuzoa kura 36,000,” alisema.

Bw Ali ambaye anauguza jeraha la mguu alilolipata wakati wa michezo ya Wabunge wa Afrika Mashariki mwaka jana, alisema baada ya kumaliza hatamu ya pili kama mbunge analenga kiti cha ugavana ili kubadilisha Mombasa.

Mbunge huyo alisema anasikitika kwamba baada ya kukipigia debe chama tawala kazi na kujitolea mhanga, kuna watu ambao wanaleta vurumai na hata kumshtumu kwamba ni mwandani wa Bw Gachagua.

“Sitoacha uswahiba wangu na Bw Gachagua ambaye alikuwa mwanachama wa UDA. Si hata leo Rais Ruto anaongea na kinara wa ODM Bw Raila Odinga? Siasa si uadui. Sitokubali kurithi uadui wa kisiasa. Kuna wale ambao wanasema mimi ni mwandani wa Bw Gachagua ili kunikandamiza kisiasa…hamtafaulu,” alisema.

Bw Ali alimsihi Rais Ruto kutatua mgogoro katika chama chake kabla maji kuzidi unga. Alisema haogopi kufurushwa kwenye chama hicho akisema haitokuwa mara ya kwanza. Alisema alijiondoa kwenye uchaguzi wa chama wikendi iliyopita akiutaja kuwa na mapendeleo.

“Hakukuwa na haki…watu kadhaa walichaguliwa na kupewa vyeti. Mimi pamoja na wafuasi wangu tuliamua kujiondoa. Huo haukuwa uchaguzi bali sarakasi. Watu wameweka vikaragosi vyao kwenye viti hivyo,” alisema.

Alisema hakuna demokrasia katika chama tawala.

“Inasikitisha kuwa wale ambao walipigania chama hiki wamebanduliwa sababu hawaabudu watu. Mimi namuogopa Mungu pekee, siogopi mwanadamu mwenzangu. Chama cha UDA kimepoteza mwelekeo,” aliongeza.

Alisema hakuna mtu atamzuia kuzungumza na Bw Gachagua.

Bw Ali alisema wakenya wanataka kiongozi anayewafanyia kazi na kuleta maendeleo. Alimsihi Rais Ruto kutimiza ahadi alizotoa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Alimuonya Rais Ruto, akisema wakenya wana ghadhabu.

“Utawekwa kwa mizani kulingana na miradi ya maendeleo uliyoanzisha…Rais Ruto tafadhali timiza ahadi ulizotoa,” alisema.