Ongezeko la halijoto linavyosambaratisha uchumi wa baharini
UNAPOKARIBIA kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume katika kisiwa cha Zanzibar, hauna budi ila kufurahia mandhari murwa ya umaridadi wa miti ya minazi inayoonekana kwa umbali.
Kisha baadaye, unapopata fursa ya kutembelea vijinjia katikati ya mji mkongwe wa Stone Town, basi bila shaka unaelewa kwa nini kisiwa hiki ni kivutio cha watalii wa mbali na karibu.
Lakini kando na vivutio hivi, kingine unachokumbana nacho hapa ni joto kali. Kama sehemu zingine katika eneo la Afrika Mashariki, kisiwa cha Zanzibar kimekuwa kikikabiliwa na ongezeko la halijoto.
Japo kisiwa hiki tokea jadi kimekuwa kikikumbwa na joto, katika miaka ya hivi majuzi, viwango vya halijoto vimekuwa vikiendelea kuongezeka.
Kulingana na Shirika la utabiri wa hali ya Anga ulimwenguni (WMO), eneo la Afrika Mashariki limekuwa likishuhudia ongezeko la viwango vya halijoto katika kipindi cha karne moja iliyopita, na hali hii imekuwa ikiongezeka katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.
Kwa mujibu wa shirika hili, halijoto ya maji ya bahari kwenye ufuo wa kisiwa cha Zanzibar, pia imekuwa ikiongezeka kwa takriban nyusi 7°C tangu mwaka wa 1990, huku halijoto baharini ikiongezeka kutoka wastani wa nyusi digrii 31°C mwaka wa 1990, hadi nyusi digrii 38°C kufikia mwaka wa 2020.
Lakini janga hili halijashuhudiwa tu kwenye kisiwa hiki pekee. Hata katika mataifa jirani kama vile Kenya, Tanzania, na Uganda, tatizo la ongezeko la halijoto, linaendelea kuwa sugu.
Kulingana na Dkt Joyce Kimutai, mwanasayansi wa tabianchi na mtafiti wa masuala ya tabianchi katika Shirika la utabiri wa hali ya anga nchini (KMS), na chuo cha Imperial College jijini London, nchini Uingereza, hali hii inaashiria hatari katika eneo la Afrika Mashariki.
“Ongezeko la viwango vya halijoto linaendelea kuchochea vimbunga,” Dkt Kimutai aeleza, “Vimbunga hivi vinaendelea kuwa na nguvu na mara nyingi kusababisha maafa katika pwani yote ya Afrika Mashariki na visiwani. Mchanganyiko wa upepo mkali, vimbunga na mvua kali vinaendelea kusababisha maafa na kuharibu miundomsingi katika eneo hili,” aongeza.
Athari kuu ya ongezeko la viwango hivi vya halijoto inaendelea kushuhudiwa katika sekta ya uchumi wa baharini katika eneo hili.
Bw Ghaamid Abdulbasat, mtaalam wa masuala ya tabianchi na viumbehai katika Muungano wa kimataifa wa kuhifadhi viumbe (IUCN), katika eneo la Afrika Mashariki na Kusini, anaangazia athari za hali hii katika mazingira ya baharini.
“Viwango vya halijoto ambavyo vimeendelea kuongezeka vimekuwa vikisababisha uchubukaji wa matumbawe, upungufu wa idadi ya samaki, huku jamii zinazoishi katika maeneo ya pwani zikiendelea kuhangaika,” aeleza Bw Abdulbasat.
Kwa mfano, Bw Pius James, Msimamizi katika kampuni ya Mwani, inayohusika na kilimo cha mwani (sea moss) na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na zao hili katika ufuo wa Paje, kisiwani Zanzibar, aeleza kwamba kutokana na ongezeko hili, wamekuwa wakishuhudia upungufu wa mazao.
“Hii ni kwa sababu joto jingi majini huchochea magonjwa kama vile ya bakteria na ukuvu, na hivyo kuathiri mimea yetu,” aongeza.
Pia humu nchini Kenya, athari hizi zinashuhudiwa, huku mimea kama vile nyasi za baharini zikiendelea kuathirika pakubwa.
Takwimu za utafiti wa uliofanywa mwaka wa 2018, zilionyesha kwamba kati ya asilimia mbili na saba ya nyasi za baharini ulimwenguni kote, zimekuwa zikitoweka duniani kila mwaka, kutokea mwaka wa 1986 hadi mwaka wa 2016, huku Kenya ikipoteza asilimia 1.69 ya mmea huu kila mwaka.
“Nyasi za baharini ni muhimu sana katika uhifadhi wa mazingira baharini kwani huchangia pakubwa katika kufyonza gesi ya kaboni hewani, kupunguza mmomonyoko wa ufuo na kudumisha viumbehai,” asema.
Anaongeza, “Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kando na mazingira ya baharini kuharibika, pia pwani zetu zinaendelea kuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na vimbunga.”
Athari za kiuchumi zinazotokana na hali hii pia zimeendelea kushuhudiwa, huku wataalam wakihoji kuwa sekta ya utalii ni mojawapo ya zile ambazo huenda zikaathirika.
“Halijoto inapoendelea kuongezeka, huenda watalii wakaonelea haja ya kutembelea maeneo yenye baridi kidogo, na sekta ya utalii inayochangia sehemu kubwa ya kipato cha mataifa ya eneo hili, huenda ikaathirika moja kwa moja kutokana na mabadiliko ya tabianchi,” aeleza Bw Abdulbasat.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, kuna baadhi ya hatua ambazo baadhi ya serikali za eneo hili zimekuwa zikichukua. Kwa mfano, katika kisiwa cha Zanzibar, serikali imekuwa ikiimarisha miundo misingi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tumekuwa tukishughulikia miradi ya uhifadhi wa maji na uimarishaji wa mifumo ya usafiri. Aidha, tunashirikiana na mashirika ya kimataifa kuimarisha miradi ya kuwezesha kustahimili athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda fuo na upanzi wa miti,” aeleza Bw Ilyass Rajab Nassor, Mkuu wa kitengo cha usimamizi katika Tume ya utalii katika kisiwa cha Zanzibar.
Lakini haya yakijiri, wataalam wanatoa wito kwa serikali za mataifa ya Afrika Mashariki kuwekeza zaidi katika mifumo ya kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya pwani.
“Ili kuangazia changamoto zinazotokana na ongezeko la viwango vya halijoto, mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuwekeza mifumo thabiti, kama vile kuimarisha usimamizi wa maeneo ya pwani, kuimarisha miundo misingi ya kuhakikisha utoshelevu wa chakula, kuweka mifumo thabiti ya kutoa onyo ya mapema ya majanga haya, na kuimarisha ushirikiano,” aeleza Bw Abdulbasat.
Aidha, Dkt Kimutai anahimiza umuhimu wa kushirikisha jamii husika katika masuala haya.
“Lakini zaidi ya yote, kunapaswa kuwepo na sera za kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi ya kaboni, ambayo ni mojawapo ya zile zinazochochea ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni.”