Jamvi La Siasa

Guu ndani, guu nje ndio mchezo wa ODM na serikali

Na CECIL ODONGO April 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

VIONGOZI wa ODM wanaendelea kuonyesha mgawanyiko mkubwa huku mguu moja ukionekana ndani ya serikali na mwingine ukiikosoa serikali ushirikiano wa Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.

Kisa cha hivi punde ambapo mgawanyiko huo ulishuhudiwa ni wakati wa mazishi ya mlinzi Bw Odinga, marehemu George Oduor katika eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya.

Viongozi hao wanaovutia mirengo miwili pinzani walionyesha tofauti za wazi mbele ya Bw Odinga na Rais Ruto ambao walihudhuria kwenye mazishi hayo.

Gavana wa Siaya James Orengo na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna walitumia hafla hiyo kuonyesha upinzani wao kwa serikali jumuishi huku wakisisitiza kwamba hawatafumbia macho maovu yanayoendelea serikali.

“Mimi siwezi kuwa kibaraka kwa sababu tulipigania katiba ambayo watu wanaruhusiwa kuzungumza. Nilikuwa bunge ambalo wabunge walikuwa wakimwaambia Rais Daniel Moi kuwa hakuna mahali ataenda na angeongoza milele,” akasema Bw Orengo kwenye mazishi hayo.

“Mkiendelea kuwa kibaraka hatutakuwa na nchi. Waambieni viongozi wenu ukweli na mimi siimbi mtu kwa sababu lugha ambayo nimesikia hapa, inaashiria kuwa nchi hii inapoteza hadhi yake,

“Maendeleo ni haki yenu ya kikatiba na nawaomba mpiganie haki zenu,” akaongeza Bw Orengo.

Bw Sifuna naye aliendelea kushambulia serikali kuhusu mkataba ambao ODM ilitia saini na UDA na pia akamtaka Rais awafute kazi baadhi ya wanaopaka tope serikali yake.

“Tulikubaliana kuwa mgao kwa kaunti ni Sh450 bilioni, sasa tunaona bungeni akina Junet Mohamed wanasema ni Sh405. Tafadhali rekebisha hayo Rais,” akasema Bw Sifuna.

Seneta huyo alimtaka Rais awachukulie hatua kali wale ambao walihusika na kisa ambacho wanafunzi wa Shule ya Upili ya Butere walihangaishwa na kutupiwa vitoza machozi kwenye tamasha ya kitaifa ya muziki kule Nakuru.

Alilalamika kuwa Afisi ya Msajili wa Vyama imekata bajeti ya ODM kwa Sh42 milioni ilhali mkataba waliotia saini ulisema waheshimu sheria na katiba ya nchi.

Rais Ruto kwenye hotuba yake alimlenga Bw Sifuna na kumwaambia aendee polepole kuhusu masuala ya serikali kwa sababu hata yeye ni mwanzilishi wa ODM.

“Nimeskia Sifuna anaongea na nguvu. Wakati unaongea mambo yangu Sifuna, ujue mimi ndio mwanzilishi wa ODM so unaenda polepole kidogo,” akasema Rais.

“Sisi ndio tulianza hii kitu. Na unajua ukinisukuma sana, nitaitisha mkutano wa waanzilishi wa ODM…tukiitisha huo mkutano tutakuadhibu, sisi ambao tulianza chama. So tuendeni mossmoss (polepole).” akaongeza.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akiongea na idhaa moja mwezi uliopita, alisema kuwa kile ambacho kitamfanya aunge mkono Rais Ruto ni iwapo changamoto ambazo zinaendelea kushuhudiwa katika sekta ya elimu zimetatuliwa na maisha ya Wakenya yanayoboreshwa.

“Kwa sasa sekta ya elimu inachangamoto na kama mtu aliyehudumu kama kiongozi wa wanafunzi chuo kikuu cha Nairobi, nitaunga tu mkono Rais kama wanafunzi wanapata pesa za Bodi ya kufadhili elimu ya juu kwa wakati na kumaliza changamoto nyinginezo,” akasema Bw Owino.

Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, Kiongozi wa Wachache Junnet Mohamed na Mbunge wa Homa Bay mjini Opondo Kaluma nao wamekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono serikali jumuishi wakisema wanafanya hivyo kutokana na miradi ya maendeleo.

“Hii nchi inaongozwa na mfumo wa demokrasia ambapo uchaguzi huandaliwa kila baada ya miaka mitano. Hatuwezi kuwa na hali ambapo baadhi ya watu wanasema Ruto lazima aende, aende wapi?

“Rais unapogawanya rasilimali ya nchi, umetugawia yetu wala hatujachukua mgao wa eneo lolote,” akasema.

Bw Mohamed alisema kuwa hakuna haja ya kupiga siasa za 2027 akisisitiza watendelea kuunga mkono utawala wa sasa ili kunufaikia miradi ya maendeleo.

“Rais na Raila mmeleta Wakenya pamoja kwa kugawanya vyeo kwa njia sawa wala hatujabaguliwa. Juzi nimeona bajeti ya miaka miwili iliyopita na barabara nyingi ilitengewa eneo moja, ubaguzi wa rasilimali lazima ukome kwa sababu kila mtu analipa ushuru,” akasema Bw Mohamed.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati, Bw Odinga amewapa wanasiasa hao idhini ya kukosoa serikali ya Rais Ruto na wakati huo huo kufanya nayo kazi huku akipima mwelekeo atakaouchukua 2027.

“Hii ni siasa na Raila ni mjanga kwa sababu akiona Rais analemewa atamtoroka lakini akiona utendakazi wake umebadilika atajitapa kuwa mawaziri wake ndio walifanya kazi hiyo,” akasema Bw Andati.