Maswali yaibuka kuhusu kifo cha mwanahabari Silas Apollo
ALIYEKUWA mwanahabari wa NMG Silas Apollo, ambaye aliaga dunia kwenye ajali ya barabarani Jumatano usiku, alionja mauti kwa sababu ya kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha ya kichwa.
Majeraha hayo yalitokana na kichwa chake kugongwa na kifaa butu kutoka upande wa nyuma. Haya yalitokana na uchunguzi wa maiti uliofanyiwa mwili wa Bw Apollo jana katika Chumba cha Kuhifadhia maiti cha Nairobi.
Uchunguzi huo uliendeshwa na Mwanapatholojia wa serikali Dkt Kiwanga mbele ya wanafamilia na polisi. Mbali na majeraha ya kichwa, uchunguzi ulionyesha alikuwa amevunjika mbavu mbili.
Mwanafamilia ambaye alizungumza na Taifa Leo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Nairobi, alisema bado wameshtushwa na mauti ya Bw Apollo ambaye hadi kifo chake alikuwa akiandikia jarida la Nairobi Law Monthly.
Mwanahabari huyo ambaye amewahi kuripoti matukio kwenye runinga ya NTV pamoja na kuandikia Daily Nation, inadaiwa alifariki baada ya kugongwa na pikipiki Jumatano usiku.
Familia yake iligundua kifo chake baada ya jamaa yake kupiga simu Jumamosi ili kumjulia hali.
Hata hivyo, simu hiyo ilipokelewa na mwanamke katika Kituo cha polisi cha Kiambu ambaye alimfahamisha kuwa mwanahabari huyo alikuwa amegongwa na pikipiki kwenye barabara ya Kiambu.
Baada ya simu hiyo, mwanamke mwingine kutoka kituo hicho alimpigia jamaa yake simu na kuwaarifu kuwa Bw Apollo alikuwa amefariki.
Alimwambia jamaa huyo kuwa Bw Apollo alipelekwa katika Hospitali ya Kiambu Level 6 ambako aliaga baada ya kujeruhiwa.
Mwili wake ulihamishwa hadi Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Nairobi saa saba mchana. Kinaya ni kuwa jamaa zake walipotembelea kituo hicho, walifahamishwa kuwa Bw Apollo mwanzo alipelekwa Hospitali ya St Teresa kwenye ambulensi ndipo akahamishiwa Kiambu.
Jamaa huyo pia alishangaa kuambiwa na polisi kuwa mhudumu wa pikipiki aliyemgonga Bw Apollo alipata majeraha madogo na aliondoka hospitalini bila kuwapa maelezo zaidi kumhusu.
Familia ya marehemu inataka kufahamu kwa nini mhudumu huyo aliachiliwa ilhali yeye ndiye mshukiwa pekee kuhusiana na mauti ya marehemu.
Pia familia imesema hakuna rekodi zozote zinazoonyesha Bw Apollo alipelekwa katika hospitali ya St Teresa au ile ya Kiambu huku wakiikosoa taarifa ya polisi kwa kukinzana.