MAONI: Sifuna atahitaji kulindwa na ODM kwa jinsi Rais alimnyanyukia kwa meno ya juu
MWANDISHI mbobezi wa fasihi Shaaban bin Roberts katika riwaya yake pendwa ya Utubora Mkulima anamtaja Utubora kuwa mtu mwenye moyo jasiri, kifua cha ujasiri na kinywa fasaha.
Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna ana hizo sifa tukizingatia aliyosema katika mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa muda mrefu wa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. Ama sijui tuseme kiongozi wa ODM.
La, pengine nimekosea, kuna serikali jumuishi. Inawezekana Raila ana cheo kikubwa kupita nilivyotaja.
Ninasema chama cha ODM kimlinde mwenzao kwa sababu kadhaa.
Mwanzo, alijigamba kuwa cheo chake ni kikubwa chamani. Ni kweli, msemaji wa chama ni yeye. Pili akampasha habari Rais Ruto kuwa wandani wake wana kiherehere kwa kuvuruga mchezo wa kuigiza wa shule ya wasichana ya Butere “Echoes of War” unaoakisi hulka mbovu za siasa ovyo.
Rais Ruto alimnyanyukia kwa meno ya juu na kumkumbusha kuwa hata yeye alikuwa ODM. Kana kwamba hilo halikutosha, Ruto akasema kuwa anaweza kupanga mkutano wa kumwadhibu Sifuna. Rais anadhani Sifuna anazungumza kama cherehani. Rais Ruto ambaye ni kiongozi wa UDA alionyesha kama ana mamlaka katika nyumba ya ODM. Raila Odinga alikimya kuhusu suala hilo ambalo limekuwa sasa mjadala wa taifa.
Nilitanguliza kutaja sifa za Sifuna nikisema zinashibana na za Utubora Mkulima kwa sababu alikuwa na ujasiri kugusa maeneo wanayoogopa wengi.
Alikuwa akiukosoa utawala wa Ruto mbele yake na pamoja na mkuu wake Raila Odinga. Alitumia hekima nyingi kupaaza ujumbe huo na kwa ufasa mkubwa.
Hata hivyo, ujasiri wake huo huenda ukamchongea katika serikali hii jumuishi.
ODM inatakiwa kuwa macho mgeni ama mpangaji wa zamani anapoiambia kuwa ipo siku wataitisha mkutano na kumwadhibu katibu wake mkuu ambaye kosa lake kubwa ni kuwa ujasiri wa kifua, mdomo unaoshusha hoja za kuwaajabisha wakuu na wadogo kwa umbo na umri, kuwa na akili yenye hekima ya kutambua ni wapi unasema nini kwa malengo yepi.
Ujumbe wa Sifuna ni kama tamthilia iliyosukwa kwa vitushi kamilifu na dhamira na maudhui yakajisimamia kwa wasomaji na wahakiki.
Sifuna alisema aliyosema kwa niaba ya chama cha ODM. Mashambulizi aliyokuwa akipata ni kwa ajili ya msimamo wa chama.
Wakuu wa ODM wangekuwa wametoa taarifa yao kuhusu matamshi ya Rais kwa katibu wao mkuu.
Vinginevyo wataonekana kuwa walikubaliana kimahubiri na matakwa ya Rais ambaye anaweza kusawiriwa kuwa mtu anayetaka kuathiri mfumo wa maamuzi ya ODM.
Wapo Sifuna wachache mno katika Kenya ya leo.
Watu wanaosema mambo kwa dhati ya nyoyo zao huhesabu vidole vyako vya mkono ukavimaliza.
Paul Nabiswa ni Mhariri wa NTV