Habari

Serikali kukohoa Sh800 milioni kujenga uwanja wa kuandaa Mashujaa Day Kitui

Na BONFACE KANYALI April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI itatumia Sh800 milioni katika kipindi cha miezi sita kubadilisha uwanja wa Ithookwe ulioko viungani mwa mji wa Kitui kuwa wa kimataifa, kabla ya sherehe za kitaifa za Mashujaa Dei zitakazofanyika Oktoba 20 mwaka huu.

Waziri wa Michezo Salim Mvurya alithibitisha hatua hiyo wakati wa ziara ya kukagua eneo hilo akiwa na Gavana wa Kitui, Dkt Julius Malombe.

Kwa kawaida, uwanja huo, hutumika kwa Maonyesho ya Kilimo ya Kaunti ya Kitui.

“Huu uwanja utakuwa na uwezo wa kuketi watu 10,000. Tunaujenga kwa viwango vya kimataifa ili uweze kutumika kwa hafla za kitaifa na kimataifa, si kwa Mashujaa Dei pekee,” alisema Mvurya.

Alieleza kuwa zabuni ya ujenzi huo itatangazwa Jumanne ijayo na kazi itaanza mara moja ili kukamilika kabla ya tarehe ya sherehe.

“Tuna tarehe ya mwisho. Kazi lazima ikamilike kabla ya Oktoba 10, ili mwanakandarasi aweze kukabidhi uwanja kwa matumizi ya sherehe ya kitaifa,” aliongeza.

Waziri huyo alifafanua kuwa uwanja huo utakuwa na paa linalozunguka sehemu zote na baada ya Mashujaa Day, serikali itaongeza miundombinu zaidi kama vile viwanja vya riadha na michezo ya soka.

Gavana Malombe kwa upande wake alihakikishia wakazi kuwa Maonyesho ya Kilimo hayatavurugwa licha ya ujenzi huo, na kusema kuwa kaunti tayari ina mipango mbadala ya kufanikisha maonyesho hayo katika maeneo mengine.

“Kwa mfano, tunaweza kuyahamishia maonyesho hayo katika eneo la viwanda la Kanyonyoo, ambako kuna nafasi ya kutosha,” alisema.

Malombe pia alimshukuru Rais William Ruto kwa kuchagua Kitui kuwa mwenyeji wa sherehe za Mashujaa Dei mwaka huu.

“Kwa niaba ya wakazi wa Kitui, namshukuru Rais kwa heshima hii. Kupitia tukio hili, tumepata uwanja wa kisasa ambao utakuwa wa manufaa kwa maendeleo ya michezo na uchumi wetu,” alisema gavana huyo.