Wanafunzi kufunzwa jinsi ya kujiliwaza kupambana na pandashuka za maisha
MASHIRIKA Na PETER MBURU
SHULE za msingi na upili nchini Uingereza zitaanza kuwapa watoto mafunzo ya kujiliwaza katika mazingira tulivu na kufungia nje ya akili kelele za ulimwengu kama mbinu ya kuwasaidia kupambana na presha zilizokuja na maisha ya sasa.
Hali hiyo inatarajiwa kusaidia afya ya kiakili ya wanafunzi, na tayari shule 370 za msingi na upili ambazo zitafanyiwa mafunzo ya majaribio zimebainishwa.
Mafunzo ya majaribio yanatarajiwa kuendeshwa hadi mwaka 2021. Mafunzo hayo yatajumuisha kuwafunza wanafunzi kuhusu mbinu bunifu kama za kutuliza akili, mazoezi ya kupumua na kujali ili kuwasaidia kudhibiti hisia, idara ya Elimu ikasema.
Wanafunzi aidha watakuwa na vipindi vya mafunzo na wataalam wa afya ya akili.
Mazoezi hayo yananuiwa kuwafanya watoto kuelekeza akili kuwaza kuhusu mambo yaliyoko kwa wakati huo pekee, badala ya kushtuka na kujuta.
“Kama jamii, tumeamua kujifungua kuhusu masuala ya afya ya akili kuliko wakati wowote mwingine ule. Lakini dunia ya sasa imeongeza presha dhidi ya watoto, huku hali kwingine ikizidi kuharibika,” katibu wa wizara hiyo Damian Hinds akasema.
Mafunzo hayo yataongozwa na shirika la Anna Freud National Centre for Children and Families kwa ushirikiano na chuo kikuu cha London.
“Tunawataka watoto na watu wa umri mdogo, wazazi na walimu kuwa na uhakika kuwa afya ya akili kwa watoto wawapo shuleni iko shwari,” akasema Dkt Jessica Deighton, mkuu wa utafiti huo.
Mradi huo unakuja wakati mtaala wa mafunzo ya lazima kuhusu afya ulianzishwa shuleni, ambao pia unahusisha afya ya akili.
Vilevile, unakuja wakati kumekuwa kukishuhudiwa chimbuko la matatizo mengi ya afya ya akili dhidi ya watoto na matineja, hali ambayo imehusishwa na masuala ya intaneti.
Utafiti uliofanywa majuzi ulionyesha kuwa upweke miongoni mwa vijana umeongezeka zaidi, haswa kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wingi.
Utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 58 ya watoto wa umri wa kati ya miaka tisa na 16 wakati mwingine huhisi upweke, idadi ya juu kutoka asilimia 51 ya mwaka jana.
Utafiti huo ambao ulihusisha wanafunzi 2000 ulionyesha kuwa wasichana wa umri mkubwa haswa walikuwa wameathirika sana, huku asilimia 80 ya wale walio na kati ya miaka 15-16 wakipambana na hali ya upweke.