Bunge kuchunguza kamari maarufu ya Aviator
BUNGE la Kitaifa limeanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za kampuni za kamari katika juhudi za kukabiliana na janga hili linalowatesa vijana wengi nchini Kenya.
Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango ya Kitaifa inatarajiwa kuwasilisha ripoti kuhusu shughuli za kampuni hizo wiki ijayo, huku wabunge wakitaka maelezo ya kina kuyahusu.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, alielekeza kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo, Kimani Kuria, kuwasilisha ripoti hiyo Alhamisi ijayo, akielezea masikitiko yake kuwa kamari imeathiri watu wengi nchini.
“Nawajua watu ambao wameathiriwa na kamari hii. Kamati hii inapaswa kujitahidi na kuwasilisha ripoti katika Bunge hili wiki ijayo,” alisema Wetang’ula.
Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Gilgil, Martha Wangari, aliyetaja mchezo wa kubahatisha uitwao Aviator, ambao alisema unatangazwa sana kwenye mojawapo ya vituo maarufu vya redio nchini.
Bi Wangari alisema kamari ya Aviator imekuwa ikitangazwa sana katika vyombo vya habari vya humu nchini, na sasa inaharibu maisha ya familia mijini na vijijini.
Alisema ingawa mchezo huo unajulikana sana miongoni mwa vijana, pia wanaume na wanawake wengi wamezama humo.
Wabunge wameeleza wasiwasi wao kuhusu visa vya wanafunzi kutumia karo yao ya shule kucheza kamari na wazazi kutumia akiba zao kujaribu bahati.
Mbunge huyo alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la usajili wa kampuni za kamari nchini katika siku za hivi karibuni, huku matangazo ya kamari yakionyeshwa kwenye televisheni.
“Huu mchezo wa kubahatisha uitwao Aviator, ambapo ndege ya kidijitali huruka na kubeba dau la mchezaji, unalewesha vijana, wanawake na watu wa rika zote, na umeharibu maisha ya wengi,” alisema.
Wabunge walisema michezo hii ya kubahatisha inayoonyeshwa kwenye runinga za humu nchini huahidi ushindi wa papo kwa papo bila juhudi yoyote, na mchezaji hahitaji kuwa na ujuzi wowote wa soka au timu yoyote ili kushiriki.
Katika uchunguzi wa Kamati ya Fedha, wabunge sasa wanataka serikali kufafanua hali halali ya mchezo wa Aviator nchini, kiwango cha ushuru na mapato yanayokusanywa kutokana na shughuli za kamari.
Pia wanataka takwimu kutoka kwa Wizara ya Mipango kuhusu kiasi ambacho Wakenya hutumia kila mwaka katika kamari na michezo ya kubahatisha.
Kamati hiyo pia itaarifu Bunge kuhusu hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Kudhibiti Kamari kudhibiti matangazo ya michezo ya kubahatisha kama Aviator kwenye vyombo vya habari vya sauti, picha na maandishi.