Ruto asimamisha kazi Mishra sakata ya figo ikichunguzwa
RAIS William Ruto amemsimamisha kazi Dkt Swarup Mishra kama mwenyekiti wa bodi ya Kenya BioVax Institute kufuatia madai ya upandikizaji haramu wa figo katika hospitali ya Mediheal, Eldoret.
Dkt Mishra, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kesses, aliteuliwa kushikilia wadhifa huo Novemba 22, 2024 na ameondolewa miezi sita baadaye uchunguzi ukiendelea dhidi ya hospitali hiyo aliyoanzisha.
Katika taarifa rasmi, Rais Ruto alisema mbunge huyo wa zamani atasimamisha kazi hadi uchunguzi kuhusu madai mazito ya ukiukaji wa maadili na shughuli haramu utakamilika.
Rais pia alisisitiza dhamira ya serikali kupambana na ufisadi na kulinda uadilifu katika sekta ya afya.Taasisi ya Huduma za Damu na Upandikizaji (KBTTS) iligundua ‘shughuli za kutiliwa shaka’ katika upandikizaji figo, ukiwemo ushiriki wa madaktari wa kigeni, na wachangiaji figo kutoka Azerbaijan, Kazakhstan na Pakistan.