Papa Francis kuzikwa Jumamosi
OFISI ya Habari ya Vatican imetangaza kuwa misa ya wafu ya Papa Francis itafanyika Jumamosi, Aprili 26, 2025, saa nne asubuhi katika St Peter’s Square, Vatican kabla ya kuzikwa alivyoagiza.
Ibada hiyo itahudhuriwa na viongozi wa Kanisa Katoliki kutoka pande zote za dunia, akiwemo Kadinali Giovanni Battista Re, ambaye ni mkuu Baraza la Makadinali, atakayesimamia ibada hiyo ya kihistoria.
Misa hiyo itashirikisha Makadinali, Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Mapadre kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.
Misa hiyo itahitimishwa na taratibu mbili za mwisho kwa heshima ya papa: Ultima commendatio (sala ya mwisho ya kumkabidhi marehemu kwa Mungu) na Valedictio (sala ya kuagana rasmi na Papa).
Baada ya misa, mwili wa marehemu Papa Francis utapelekwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro (Basilica), kabla ya kusafirishwa kwenda St Mary Major Basilica kwa mazishi, kama alivyoagiza kwenye agizo lake la kiroho (wosia wa kiroho).
Kabla ya mazishi, mwili wa Papa Francis utasafirishwa kutoka kasri la Casa Santa Marta hadi Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mnamo Jumatano, Aprili 23, kuanzia saa tatu asubuhi katika tukio litakaloanza kwasala ya pamoja.
Ibada hiyo ya kusindikiza jeneza itaongozwa na Kadinali Kevin Farrell, ambaye ni Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma.
Msafara wa jeneza utapita katika Uwanja wa Santa Marta na Uwanja wa Wafiadini wa Roma wa Kwanza (Roman Protomartyrs), kabla ya kupitia Lango la Kengele (Arch of the Bells) hadi uwanja wa St Peter’s Square.
Mwili wa Papa utawekwa katika eneo la Altari ya Maungamo (Altar of the Confession) ndani ya Basilica. Baada ya ibada, waumini na viongozi mbalimbali wataruhusiwa kutazama mwili wa Papa kutoa heshima za mwisho
Mazishi ya Papa Francis yanatarajiwa kuleta pamoja viongozi wa dini na mataifa, pamoja na mamilioni ya waumini duniani kote, wakikumbuka maisha ya Papa aliyekuwa kielelezo cha amani, upendo kwa waliopuuzwa, na mshikamano wa dunia.