Trump kuuongoza ulimwengu katika mazishi ya Papa Francis
VATICAN CITY
PAPA Francis atazikwa Jumamosi hii St Peters Square, makadinali wa Kanisa Katoliki jijini Roma, Italia jana waliamua.
Tangazo hilo lilipisha kuanzishwa kwa mchakato wa kumpa Papa Francis mazishi ya heshima huku viongozi mbalimbali mashuhuri ulimwenguni wakitarajiwa kuhudhuria.
Ibada ya mazishi ya Papa Francis itaanza saa nne asubuhi Jumamosi na inatarajiwa kuhudhuriwa na marais wengi na viongozi wa hadhi ya juu ulimwenguni.
Rais wa Amerika Donald Trump ambaye alikuwa akitofautiana vikali na Papa Francis kuhusiana na sera ya utawala wake kuhusu uhamiaji, jana alisema atahudhuria ibada hiyo pamoja na mkewe.
Viongozi wengine ambao walikuwa wamethibitisha kuhudhuria mazishi hayo ni Javier Milei, Rais wa Argentina alikozaliwa Papa Francis, Luiz Lula (Brazil) na Volodymyr Zelenskiy (Ukraine).
Papa Francis alikuwa amesema azikwe katika kanisa la Basilica ya St Mary Major badala ya St Peters ambako wengi wa mapapa walioaga hapo awali wamekuwa wakizikwa.
Jana Vatican ilitoa picha zilizoonyesha mwili wa Papa Francis ukiwa umewekwa kwenye jeneza la mbao katika jumba la Santa Marta ambako aliishi kwa miaka 12.
Walinzi kutoka Uswisi walisimama kila upande wa jeneza hilo. Mnamo Jumatano asubuhi, mwili wake utapelekwa St Peter’s Basilica saa tatu mchana kwenye msafara ambao utaongozwa na makadinali.
Waumini wa kanisa Katoliki watakuwa na nafasi ya kutazama mwili huo na kutoa heshima zao za mwisho kwa Papa Francis ambaye alikuwa papa wa kwanza kutoka Latin Amerika.
Makadinali wote jijini Roma waliagizwa wafike kwenye mkutano wa jana ili kuamua utaratibu ambao utafuatwa kuelekea mazishi ya Papa Francis.
Pia walizungumzia jinsi ambavyo shughuli za kanisa Katoliki zitakavyoendelea kabla ya papa mwingine kuchaguliwa.
Mchakato wa kumteua papa mpya huchukua kati ya siku 15-20 baada ya mauti ya papa aliyekwepo. Hii ina maana kuwa mchakato huo unastahili kuanza Mei 6.
Makadinali 135 watapiga kura ya siri ambayo inaweza kuendelea kwa siku kadhaa. Moshi mweupe kutokea kwenye mvuke wa kanisa la Sistine ni ishara kuwa papa mpya amepatikana na kwa Papa Francis, hakukuwa na kiongozi ambaye alionekana kuwa kifua mbele kumrithi.
Papa Francis, 88, aliaga dunia mnamo Jumatatu kutokana na ugonjwa wa kiharusi na wa moyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vatican.
Papa alikuwa hospitalini kwa wiki tano mapema mwaka huu akiugua maradhi ya pumu na nimonia.
Alirejea Vatican mwezi mmoja uliopita na alionekana kuimarika kiafya na hata akaongoza Misa ya Pasaka mnamo Jumapili katika eneo la St Peter’s Square.