Habari za Kaunti

Serikali yafunga kanisa la mauti baada ya wawili kufariki

Na GEORGE ODIWUOR April 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI imeagiza kufungwa kwa kanisa la Malkio St Joseph Mission of Messiah in Africa lililoko kijiji cha Opapo, Kaunti ya Migori, kufuatia vifo vya kutatanisha na ripoti za hali mbaya ya maisha ndani ya uwanja wa kanisa.

Kamati ya usalama ya kaunti ndogo ya Rongo, ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo, Bw George Matundura, iliagiza kufungwa kwa kanisa hilo kwa  usalama wa waumini na jamii.

“Tumesitisha shughuli zote za kanisa hili. Eneo hilo sasa halifai kuwa na watu na kila mtu anahamishiwa  maeneo salama,” alisema Bw Matundura.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kifo cha Bw Elly Odoyo, aliyekuwa mkazi wa zamani wa Magwagwa, Kaunti ya Nyamira, ambaye aliishi katika kanisa hilo kwa takriban miaka ishirini.

Bw Odoyo alifariki Jumatatu, Aprili 21, kutokana na majeraha aliyoyapata katika mzozo ulioripotiwa kutokea ndani ya kanisa hilo. Familia yake inasema alikuwa amekatiza uhusiano nao kwa miaka mingi, na alikuwa akiwapigia simu mara chache tu kuomba msaada wa kifedha.

Kulingana na kaka yake, Bw Isaac Nyachieo, Bw Odoyo aliwahi kujaribu kuuza ardhi yake akidai alitaka kulipia karo watoto wake, lakini familia ilikataa na kumshauri aihifadhi kwa urithi wa watoto hao.

Licha ya juhudi za kuwasiliana naye, familia haikuruhusiwa kuingia kanisani. Walielezwa kuwa alikuwa amesafiri kwenda tawi la kanisa hilo huko Seme, Kaunti ya Kisumu. Walipokea simu kutoka kwa binti yake Jumapili iliyopita wakiarifiwa kuwa alikuwa mgonjwa mahututi, lakini walipofika, walipata akiwa tayari amefariki.

Kifo hicho kilichochea uchunguzi wa shughuli za kanisa hilo, na Jumatatu usiku, polisi walifanya msako na kuwaokoa watu 57, wakiwemo watoto wa kuanzia miaka mitano.

Mapema mwezi huu, familia moja kutoka Kisumu ilivamia eneo hilo kwa nguvu ili kufukua mwili wa jamaa yao, afisa wa Kikosi cha Kukabiliana na Fujo (GSU) aliyefariki na kuzikwa ndani ya kanisa siku moja tu baada ya kifo chake. Tukio hilo lilizua ghasia na sehemu ya ukuta wa kanisa ilibomolewa na wananchi waliotaka kujua kilichoendelea ndani ya eneo hilo.

Wakili wa kanisa hilo, Bw Bernard Achola, ameapa kushtaki serikali mahakamani kwa kufunga kanisa hilo. Anasema hatua hiyo imekiuka haki za waumini, wengi wao wakiwa wamezaliwa na kulelewa humo na hawana makazi mengine.

“Kanisa hili limekuwepo tangu miaka ya 1970 na limesajiliwa rasmi. Waumini wengine hata waliuza au kuchangia ardhi yao kwa matumizi ya kanisa,” alisema Bw Achola.

Hata hivyo, serikali inasisitiza kuwa hali mbaya ya maisha, kupinga matibabu ya kawaida, na vifo vya kutatanisha kunahitaji hatua ya haraka kuchukuliwa.

Maafisa wa afya ya umma waliokagua eneo hilo waliripoti hali mbaya ya usafi na usalama.

Kwa sasa, eneo hilo ambalo hapo awali lilikuwa na shughuli nyingi limebaki kimya, wanyama wakizurura huku mali ya watu ikiwa imesambaa kila mahali.