Wazee wa Kaya wadai Spika Kingi anaingilia ajira za bandari
BAADHI ya Wazee wa Kaya kutoka Kaunti ya Kwale wamemnyoshea kidole cha lawama Spika wa Bunge la Seneti, Amason Kingi, wakidai anapanga njama ya kumwondoa mamlakani Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA), Benjamin Dalu Tayari.
Wazee hao wa Mijikenda walimtaka Bw Kingi kukoma kuingilia kazi ya Bw Tayari na badala yake kujihusisha na masuala ya Bunge la Seneti.
Walimtetea Bw Tayari wakisema anafaa kuendelea na kazi yake wakisisitiza ameleta mabadiliko bandarini hususan ile ya Mombasa.
Wakiongozwa na Mzee Juma Mwakiroho, wazee hao walisema muhula wa mwenyekiti huyo unafaa kuongezwa.
Wenzake ambao ni wakazi wa Kwale akiwemo Patrick Mangale pamoja na mwenzake Daniel Kitsao, walidai kuwa Bw Kingi ameshirikiana na wanasiasa wengine kumhujumu Bw Tayari.
Wakiongea na wanahabari katika bustani ya Mama Ngina, Kaunti ya Mombasa, wazee wa kaya na baadhi ya wakazi wa Kwale walisema wanamtetea Bw Tayari kutokana na rekodi yake ya utendaji kazi ambayo imeimarisha utendaji kazi wa bandari ya Mombasa.
“Tunashangaa Bw Kingi ana nia gani ya kupinga kuongezwa kwa muhula wa mwenyekiti wa bandari za humu nchini. Inaonekana anataka kuweka mtu wake katika nafasi hiyo,” alisema Bw Mangale.
Aliongeza kuwa mtangulizi wa Bw Tayari, Joseph Kibwana, alitoka Kaunti ya Kilifi na alihudumu bila kutatizwa katika kipindi chote cha uongozi wake.
“Tulimuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti kutoka Kilifi, na sasa Bw Kingi anafaa kutuunga mkono pia sisi wa Kwale,” aliongeza Bw Mangale.Walimshutumu Bw Kingi kwa kutumia wadhifa wake serikalini na kama kinara wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kuvuruga shughuli za usimamizi wa bandari.
Hata hivyo, usimamizi wa PAA ukiongozwa na Katibu Mkuu, Kenneth Tungule, ambaye pia ni Mbunge wa Ganze, alipinga madai hayo akiyataja kuwa porojo na uzushi tu.
“PAA inazidi kushika kasi katika Kaunti ya Kwale na hii imeanza kuzua hofu miongoni mwa baadhi ya viongozi wa kisiasa eneo hilo,” alisema Bw Tungule.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mbunge huyo alisema wanasiasa wengine wameanza kushikwa na kiwewe kufuatia umaarufu wa PAA.
“Ili kukabiliana na umaarufu wa PAA unaokua kwa kasi katika kaunti hiyo, baadhi ya wanasiasa wamebuni mpango wa kudhalilisha chama hiki machoni pa wakazi wa Kwale. Wanataka kuifanya PAA kuwa adui wa watu wa Kwale,” alisema Bw Tungule akishikilia kuwa Bw Kingi hana njama ya kuingilia nafasi ya Bw Tayari.
“Wanadhania kuna njama ya kumuondoa Bw Tayari na kumweka mamlakani Bw James Mulewa ambaye anatoka Kilifi na aliwahi kuwa mkurugenzi mkuu,” alisema mbunge huyo.Bw Tungule alisema Spika wa Bunge la Seneti wala PAA hawana ushawishi wa kuondolewa kwa Bw Tayari.
“Chama cha PAA kitajivunia kuona Bw Tayari akiongezewa muhula mwingine,” alisema. Bi Mwaka Kibwana ambaye pia ni mzee wa Kaya alisema Bw Kingi hafai kuingilia maswala ya uongozi wa bandari bali kumuunga mkono Bw Tayari ambaye ni mpwani