MAONI: Waafrika waanze kujipigania kivyao kwa sababu Trump hana muda wala nia
SIKU hizi mambo yakimwendea vibaya Mwafrika anakimbia kumlaumu Rais Donald Trump wa Amerika, hata kuhusiana na mambo ambayo kamwe hana mwao nayo.
Hata kina ‘pangu pakavu tia mchuzi’ mitaani wanateta kwamba dawa za kukabiliana na makali ya Ukimwi zimekosekana kwa kuwa kiongozi huyo wa chama cha Republican amezuia misaada, kwa hivyo dawa hizo hazinunuliki.
Naambiwa hata kwenye shoroba za kisiasa, viongozi wa mataifa ya Afrika wanalalamika kwamba chumi zao zimezorota kutokana na sera mbovu za Amerika chini ya utawala wa Trump.
Hata mashoga wamo! Hivi majuzi nchini Ghana, mashoga wameinuka na kumlaumu Rais Trump kwa kile walichokiita kuwapa motisha wanasiasa wa Ghana wanaochukia kundi hilo linalofanya ngono kinyume na maumbile.
Wameteta kwamba, kutokana na ujio wa pili wa Rais Trump, wanasiasa wa taifa hilo la Afrika Magharibi wamejasiria kurejesha bungeni mswada mkali dhidi ya mashoga kwa nia ya kuupitisha ili uwe sheria ya nchi.
Mswada huo ulipitishwa mwaka jana, lakini aliyekuwa rais wa Ghana wakati huo, Nana Akufo-Addo, hakuutia saini kuuidhinisha kuwa sheria, hivyo muda uliotengewa kisheria umepita.
Mashoga na wanaharakati wao wanahofia kwamba mswada huo ukipitishwa tena wakati huu ambapo Trump yupo madarakani, Rais John Mahama atausaini bila kusita na kuanza kuwaadhibu mara moja.
Mashoga na wanaharakati wao nchini Uganda, ambako tayari kuna sheria kali dhidi yao, pia wameelezea hofu yao kwamba huenda hawatakuwa na mtetezi kwa sababu Rais Trump anaonekana kutojali lolote linalofanyika nje ya Amerika.
Nimelazimika kujiuliza maswali kadha: Kuna hekima gani kwa Waafrika kumtegemea kiongozi wa Amerika hata katika masuala ya ngono? Je, utegemezi huo, ambao bila shaka ni ukoloni mambo-leo, haumfanyi Mwafrika kiumbe dhaifu kisichojipigania?
Ni sahihi kuwa Rais Trump ana shughuli nyingi, hataweza kuwasaidia. Kiongozi huyo matata yuko shughulini kubomoa asasi za serikali ya nchi yake kama zinavyojulikana tangu zamani.
Na, kwa kuwa katika harakati zake hizo anakabiliwa na changamoto za kisheria, hana muda wa kupoteza na masaibu madogo-madogo yanayowasibu wakazi wa mataifa yanayoendelea.
La ziada ni kwamba Trump mwenyewe anawaiga viongozi wa Afrika ambao wana mazoea ya kupuuza maagizo ya mahakama kwa kuwa mengi yanatolewa dhidi yake, na haamini ‘mfalme’ kama yeye anapaswa kuzuiwa kufanya chochote.
Maskini Mwafrika, ukitaka ithibati kwamba Trump hana muda wa kupoteza akishughulikia matatizo yanayokukabili, watafute majirani zako ambao awali walifanya kazi na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Amerika (USAID).
Mahakama ilikwisha kuamua kwamba uamuzi wa kulivunjilia mbali shirika hilo, ambao ulitolewa na Trump, ulikuwa kinyume cha sheria, lakini mkaidi huyo anaendelea kujitia hamnazo.
Tayari serikali ya Trump inazozana na mahakama kuhusu hatua ya kuwaondoa wakazi wa Amerika na kuwapeleka nchi za watu kinyume cha sheria. Mahakama imeamua walioondolewa warejeshwe, lakini serikali ya Trump imekataa.
Mahakama imeagiza serikali hiyo ibatilishe uamuzi wa kulivunjilia mbali shirika la habari la Sauti ya Amerika (VOA) na sasa wadau wengi wanasubiri kwa hamu na ghamu kuona iwapo itatii agizo hilo au itafanya kama serikali za Afrika.
Usitafute mifano serikali tundu mbali; Kenya imepuuza maagizo kadha ya mahakama. Tabia hiyo mbaya ilianzishwa wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta, na imeigwa vizuri tu na utawala wa Rais William Ruto.
Kama ripota wa zamani wa mahakama, uamuzi wa serikali yoyote ile kutotii maagizo ya mahakama hunipa hofu kwa kuwa inawaonyesha raia wake kwamba mtu anaweza kuvunja sheria na akakataa adhabu.
Pole kwa wanaosubiri msaada wa aina yoyote kutoka Amerika. Huu ni wakati wa watu kujipigania wajuavyo. Pia ni fursa ya kukomaa.
Miaka 60 na ushei ya uhuru wa nchi isipowakuza mashujaa wa mapambano mapya, tunapaswa kubadili mbinu za malezi.