Gor yatathmni kujenga uwanja wake wa soka unaositiri mashabiki 60,0000 Ukambani
NDOTO ya Gor Mahia ya kumiliki uwanja wa soka inaonekana haitakawia sana baada ya uongozi wa klabu hiyo kuanza mchakato wa kukagua shamba ambako wananuia kujenga uga wenye uwezo wa kuwasitiri mashabiki 60,000.
Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Rais Eliud Owalo mnamo Alhamisi aliongoza uongozi wa Gor kutembelea shamba hilo la ekari 40 ambalo lipo karibu na Chuo Kikuu cha Daystar, eneo la Lukenya Kaunti ya Machakos.
Owalo analenga kusaidia Gor kujenga uga ambao unaweza kuwasitiri mashabiki 60,000, nyuga tatu za kufanyia mazoezi ambazo zitakuwa za Gor Mahia Youth, Gor Mahia Queens na timu ya chipukizi ya klabu hiyo.
Uga huo pia utakuwa makazi ya hadhi kwa wachezaji, hoteli ya kisasa ya kiwango cha 4 star, vyumba vya kufanyia mazoezi, afisi za klabu na chumba cha wanahabari.
Pia itakuwa pa kuogolea, duka kubwa la kuuza jezi na mali nyingine ya klabu, vyoo, eneo pana la kuegesha magari pamoja na vifaa vingine vya kisasa.
“Kama naibu mlezi wa Gor, asubuhi hii nimeongoza usimamizi wa klabu kukagua ardhi ya ekari 48 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Gor, nyumba za wachezaji na vifaa vingine muhimu,” akasema Owalo.
Aliandamana na mwenyekiti wa klabu hiyo Ambrose Rachier, Katibu Mkuu Nicanor Arum na mwekehazina Gerphas Okuku.
Owalo alikabidhiwa nafasi ya naibu mlezi wa Gor majuma mawili yaliyopita, akichukua wadhifa huo kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Homa Bay Cyprian Awiti.
Iwapo ujenzi huo utafanyika, basi Gor itakuwa klabu ya kwanza nchini ya kumiliki uwanja wa kisasa ambao unatoshana na ule wa Kasarani ambao utatumika kwa mechi za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2027.
Kutokana na juhudi za waziri huyo wa zamani wa mawasiliano na teknolojia, Gor ilinunuliwa basi lenye uwezo wa kuwabeba mashabiki 42 kwa kima cha zaidi ya Sh22 milioni.
Waziri huyo alikabidhi Gor basi hilo mnamo Novemba 2023 kwenye hafla iliyojaa bashasha tele katika uga wa Kasarani.
Gor na AFC Leopards zilipokezwa vipande vya ardhi vya kujengea uwanja eneo la Kasarani na Rais Daniel Arap Moi miaka ya 80. Hata hivyo, ardhi hizo zilinyakuliwa na kujengewa makazi huku timu hizo pia zikiwa hazina cheti cha kumiliki ardhi hizo.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wamemkosoa Owalo wakisema uga huo ungejengwa Nyanza ambako Gor ina asili yake. Wengine nao wamependekeza hadhi ya City Stadium ingeimarishwa kwa sababu ndio uga wa nyumbani wa K’Ogalo.
Wengine nao wamesema Gor ni timu inayojivunia mashabiki hata kutoka makabila mengine kwa hivyo hakuna tatizo uga ukijengwa Kaunti ya Machakos.