Gachagua: Nilikuwa nimemaliza kabisa pombe haramu Mlima Kenya lakini sasa imerudishwa
ALIYEKUWA naibu rais Rigathi Gachagua, ameonya kuhusu kurejea kwa pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya.
Akizungumza Jumatano na wakazi wa kijiji cha Kangai, Kaunti ya Kirinyaga, Bw Gachagua, alilalamika kuwa serikali ya Kenya Kwanza imeruhusu uuzaji wa pombe hatari zinazoharibu maisha ya wananchi.
“Nilipokuwa serikalini nilishinda vita dhidi ya pombe zilizokuwa zikiangamiza watu wetu, sasa pombe hizo zimerudi na zinatishia maisha ya wakazi,” alisema.
Alieleza kuwa vileo hivyo ni hatari na vinazorotesha maendeleo, na lazima viondolewe kabisa.

“Tukichukua serikali, tutahakikisha kuwa pombe hizo zenye sumu zinaondolewa sokoni,” alisisitiza.
Alizungumza baada ya watu watatu kulazwa hospitalini baada ya kunywa pombe inayoshukiwa kuchanganywa na kemikali hatari katika eneo la Kangai.
Watatu hao walilalamika kuumwa na tumbo na kizunguzungu baada ya kunywa pombe hiyo kwenye baa kijijini.
Walihamishwa kutoka kituo cha afya cha Njegas hadi hospitali ya rufaa ya Kerugoya kwa uchunguzi zaidi wa kiafya.
Mnamo Februari 5 mwaka jana, watu kumi na saba walifariki katika eneo hilo hilo huku wengine kadhaa wakipofuka baada ya kunywa pombe yenye sumu.
Tukio hilo lilishtua taifa zima huku Wakenya wakilaumu serikali kwa kulegea katika jukumu lake.
Bw Gachagua alishutumu serikali kwa kutowajali watu wa eneo la Mlima Kenya.
“Tutalinda na kuwasaidia watu wetu tukichukua mamlaka,” alisema.