Pigo kwa Timamy mahakama kuthibitisha ushindi wa Twaha
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya Juu Jumatano ilithibitisha ushindi wa Gavana wa Lamu Bw Fahim Twaha ilipotupilia mbali rufaa aliyowasilisha kupinga matokeo ya uchaguzi wake na Bw Issa Timamy.
Jaji Mkuu (CJ) David Maraga, majaji wa mahakama ya juu Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola walipitisha kwa kauli moja Bw Twaha alishinda kwa njia halali.
Na punde tu Bw Twaha alipotangazwa mshindi na Mahakama ya Juu, alitoa wito kwa Bw Timamy waungane kutoa huduma kwa wakazi wa kaunti ya Lamu.
Ushindi wa Bw Twaha aliyenyakua kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Jubilee alimshinda Gavana wa kwanza katika kaunti hiyo Bw Issa Timamy aliyechaguliwa 2013 kwa tikiti ya chama cha Amani National Congress (ANC) ambacho kinara wake ni Bw Musalia Mudavadi.
Bali na Bw Twaha mahakama hiyo ya upeo pia ilimtangaza Mbunge wa Changamwe Bw Omar Mwinyi mshindi halisi wa kiti hicho.
Wakitoa uamuzi katika rufaa hizo mbili majaji hao walisema walalamishi waliowasilisha rufaa hizo walishindwa kuthibitisha madai kwamba washindi walikaidi maadili , mwongozo na sheria za uchaguzi.
Katika kesi ya Bw Twaha majaji hao walisema Bw Timamy alishindwa kabisa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha madai ya kuvurugwa kwa sheria za uchaguzi na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kumfaidi mshindi.
IEBC ilimtangaza Bw Twaha mshindi wa kinyang’anyiro hicho cha Ugavana kwa kuzoa kura 22,969 zikiwa ni asili mia 46.57 ya wapiga kura walioshiriki katika zoezi hilo.
Bw Timamy aliimbuka wa pili kwa kuzoa kura 22,848 ikiwa ni sawa na asili mia 45.45 ya kura zilizopigwa katika vituo vya kupigia kura 167 katika kaunti hiyo.
Bw Timamy alishindwa na Bw Twaha na kura 121.
Akasema Jaji Maraga na majaji wenzake, “Ijapokuwa tofauti ya kura kati ya mshindi na mshindwa ilikuwa ni 121 hii haimaanishi uchaguzi ulifanywa.”
Bw Timamy alikuwa mmoja wa wale walioshindwa na wawaniaji wapya wa viti tofauti tofauti.
Gavana huyo wa kwanza aliwasilisha kesi ya kwanza katika mahakama kuu Malindi na ikatupiliwa mbali.
Alikata rufaa ya kwanza katika mahakama ya rufaa na majaji watatu wakaisikiza na kuitupilia mbali kwa madai kesi hiyo haikuwa na mashiko kisheria kuwezesha uamuzi wa wapiga kura kubatilishwa.
Majaji watatu wa Mahakama ya rufaa wakiongozwa na Jaji Alnashir Visram walitupilia mbali kesi dhidi ya Bw Twaha na kuamuru alipwe gharama ya Sh12 milioni.
Jaji Maraga na wenzake watano walikubaliana uamuzi wa mahakama ya rufaa na kusema “ uchaguzi wa ugavana Lamu ulifanywa kulingana na sheria za uchaguzi na hakuwa na kasoro yoyote.”
Majaji hao walitupilia mbali madai 41 kwamba kura zilitiwa alama kwingine na kuwasilishwa katika ukumbi wa kuhesabia kura.
Pia kulikuwa na madai kwamba wapiga kura walizuiliwa kushiriki katika zoezi la kupiga kura.
Bw Timamy alikuwa amedai kulikuwa na upendeleo uliotekelezwa na maafisa wa IEBC kwa lengo la kumfaidi Gavana Twaha.
Kwa ujumla Bw Timamy alikuwa amedai uozo usio na kifani ulishuhudiwa wakati wa uchaguzi huo mkuu wa Agosti 8 2017.
Bw Timamy alikuwa amedai wapiga kura walikuwa wamelambishwa hongo na mpinzani wake , madai ambayo korti ilisema hayakuthibitishwa.