Habari Mseto

WGCA yatinga fainali ya Tuzo za hadhi za SABRE Afrika 2025

Na CECIL ODONGO April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMPUNI ya mawasiliano ya Winnie Gor (WGCA), imeweka Kenya katika ramani ya Afrika baada ya kuorodheshwa kati ya kampuni ambazo zipo pazuri kutwaa Tuzo za Hadhi za SABRE Afrika 2025.

Tuzo za SABRE ni kati ya zile zinazothaminiwa sana ulimwenguni na hutolewa kwa kampuni za mawasiliano ambazo zinashirikisha uvumbuzi na kushiriki miradi au programu ambazo zinainua jamii.

Mwaka jana, Winnie Gor ilisimamia Mashindano ya kukuza soka mashinani maarufu Tujiamini Initiative ambayo ilidhaminiwa na Sportpesa. Mashindano hayo ya soka yalisaidia kutambua vipaji vya soka huku washindi pia wakitunukiwa tuzo mbalimbali.

Tujiamini Initiative imeorodheshwa kuwania tuzo hizo za hadhi kwa kubobea  kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na itahimili ushindani wa  kampuni nyingine nne kutoka mataifa mengine ya Afrika.

Pia, Winnie Gor inalenga kuleta nyumbani tuzo ya kampuni bora inayoshirikisha matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuendesha shughuli zake.

Podikasiti “Talk To Me Direct’ ya Luminate Africa ndiyo itamenyana na washindani wengine wawili kwenye kitengo cha kampuni bora ya kidijitali.

Kampuni hiyo ya mawasiliano ina nafasi kubwa ya kubeba tuzo hizo za SABRE wakati ambapo washindi watatangazwa jijini Mombasa mnamo Juni 12.

“Kuorodheshwa kati ya kampuni zinazowania ushindi ni idhibati tosha kuwa tumepiga hatua katika utendakazi wetu hasa kwenye matumizi ya teknolojia na pia uvumbuzi,” akasema Winnie Gor ambaye ni mwanzilishi wa WGCA.

“Uteuzi wetu ni zaidi ya utambuzi kwa sababu unadhihirisha ushindani mkali ambao upo Afrika,  kampuni mbalimbali zinapotumia uvumbuzi kubadilisha mawanda ya mawasiliano. Nawapongeza washindani wetu na nina matumaini na matarajio makuu wakati ambapo mshindi atakuwa akitangazwa,” akaongeza.

Kati ya kampuni ambazo Winnie Gor imekuwa  ikishirikiana nayo katika shughuli zake ni Wakfu wa Agha Khan, Corp Afrika, wakfu wa Mastercard, SNDBX, Kampuni ya Bima ya Waislamu inayofahamika kama Takaful miongoni mwa nyinginezo.