Habari Mseto

Waziri aeleza kinachofanya HELB ikose kufadhili wanafunzi wa KMTC

Na SAMWEL OWINO April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

PENGO la Sh19 bilioni katika bajeti na ukosefu wa mwongozo wa kisheria ni changamoto kuu zinazozuia wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Uuguzi Kenya (KMTC) kupata fedha moja kwa moja kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB).

Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, aliambia Kamati ya Pamoja ya Bunge ya Elimu na Afya kuwa, ingawa Wizara ya Elimu ingependa kusaidia wanafunzi wote katika taasisi za elimu ya juu, kanuni zilizopo kwa sasa haziruhusu kutoa msaada kwa taasisi zilizo nje ya wizara hiyo.

Bw Ogamba alisisitiza kuwa vyuo na taasisi za mafunzo, kama KMTC, huandaa bajeti zao kupitia wizara zao husika na sio moja kwa moja chini ya Wizara ya Elimu.

HELB hupokea bajeti yake kupitia Wizara ya Elimu, KMTC iko chini ya Wizara ya Afya.

Hii inasababisha changamoto katika ugavi wa rasilmali, hasa kwa taasisi kama KMTC ambazo ziko nje ya Wizara ya Elimu.

“Ukweli ni kwamba baadhi ya taasisi, kama KMTC, ziko chini ya Wizara ya Afya na si Wizara ya Elimu na kuna athari kubwa kwa mchakato wa bajeti unaofanywa na Bunge la Taifa,” Bw Ogamba aliambia kamati.

Kwa sababu hii, bajeti inayotolewa kwa HELB ni kwa wanafunzi katika taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Elimu, na hivyo basi, taasisi kama KMTC hazipati fedha moja kwa moja kupitia HELB, alieleza Ogamba.