Gavana Nassir ahamishia afisi yake hospitali ya umma kusimamia mageuzi
GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir amehamishia afisi yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mafunzo ya Makadara, katika juhudi za kuboresha huduma za afya ambazo zimekuwa zikikumbwa na changamoto.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, Gavana Nassir alisema atafanya kazi kutoka hospitali hiyo kubwa ya umma kwa kipindi cha wiki moja ili kusimamia kwa karibu uboreshaji unaoendelea.
“Wiki hii, nimehamishia afisi yangu hapa Hospitali ya Makadara kusimamia moja kwa moja na kuharakisha mageuzi ya huduma tunayotekeleza,” alisema katika ujumbe huo.
Sekta ya afya katika Kaunti ya Mombasa imegonga vichwa vya habari kutokana na kuzembea kwa wauguzi, kutoza ada za juu za huduma za afya, na kukosa kutoa huduma bora.
Gavana huyo alibainisha maeneo muhimu anayotilia mkazo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wauguzi, kuweka mfumo wa kidijitali katika uendeshaji wa hospitali, kuimarisha mafunzo ya wahudumu wa afya na kuongeza usimamizi ili kuhakikisha uwajibikaji.
“Afya ni haki ya kila mwananchi, na tunahakikisha huduma hii inafanya kazi kwa watu wetu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa notisi iliyotumwa kwa wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa idara ya afya, ilithibitishwa kuwa gavana huyo atakuwa akifanya mikutano na ziara katika hospitali mbalimbali za kaunti ili kufuatilia hali ya huduma kwa wananchi.
“Katika kipindi hiki, Gavana atatekeleza mikutano na kufanya ziara za ukaguzi katika vituo muhimu vya afya vya kaunti,” ilieleza sehemu ya notisi hiyo.
Miongoni mwa hospitali atakazotembelea ni pamoja na Hospitali ya Port Reitz, Tudor, Utange, Mtongwe na Makadara.
Hatua hii imejiri wakati ambapo kuna malalamiko ya umma kuhusu hali duni ya huduma za afya Kaunti ya Mombasa, huku wakazi wakilalamikia huduma hafifu na uzembe katika hospitali za umma.
Aprili mwaka huu, 2025, wagonjwa watatu waliripotiwa kufariki katika hospitali ya Makadara kufuatia hitilafu ya oksijeni, jambo lililoibua ghadhabu na wito wa uwajibikaji.
Katika tukio tofauti, msichana wa miaka 13, Victoria Hawi, alifariki dunia katika hospitali ya Port Reitz, familia yake ikidai alipuuzwa na wahudumu wa afya, jambo lililoongeza ghadhabu miongoni mwa wananchi kuhusu mfumo wa afya.
Haya si matukio ya kipekee, kwani kuna madai mengi kutoka kwa wananchi kuwa wagonjwa wengi wamekuwa wakipuuzwa au kutendewa kinyume.
Wakazi pia wamewalaumu baadhi ya wahudumu wa afya kuwa na tabia ya ukatili na kutojali, hali inayozidisha mgawanyiko kati ya umma na wahudumu wa afya.
Hata hivyo, wahudumu wa afya wamejitetea wakisema kuwa hali ya ukosefu wa wafanyakazi inawalazimu kufanya kazi kupita kiasi bila kupumzika.