Habari za Kitaifa

Urais 2027: Kalonzo atasalitiwa tena?

Na CECIL ODONGO May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ndiye mwanasiasa anayekabiliwa na kibarua kikubwa ndani ya muungano mpya wa upinzani unaosukwa ikizingatiwa amewahi kusalitiwa kwenye ushirikiano kama huo katika chaguzi za nyuma.

Wengi wanasubiri kuona mikakati ya kisiasa ambayo Bw Musyoka atachukua kujilinda iwapo hatimaye hatakuwa mpeperushaji wa bendera ya muungano huo mpya.

Muungano huo wa upinzani ambao ulianza kusukwa Jumanne, Aprili 29, 2025 unawashirikisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na Kiongozi wa PLP Martha Karua. Wengine ni waliokuwa mawaziri Justin Muturi na Mithika Linturi, huku Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akiwakilishwa kupitia chama chake cha Jubilee.

Baada ya muungano huo kubuniwa, tayari mjadala umeanza kuzuka nani kati yao atakuwa bora zaidi kumenyana na Rais William Ruto ambaye atakuwa akitetea wadhifa wake 2027.

Hii ni licha ya kwamba katika mkutano wa Jumanne, wanasiasa hao waliafikiana washirikiane, waandae mikutano ya umma pamoja kisha ikisalia miezi michache kabla ya kura, waafikiane nani kati yao atawania urais.

Hata hivyo, macho yote yapo kwa Bw Musyoka, 71 ambaye wadadisi na wandani wake wanaona kuwa 2027 ndio mwaka ambao anastahili kuwa debeni na akikosa basi atapoteza zaidi.

Mwaka 2027, Bw Musyoka atakuwa na umri wa miaka 73 na akikosa kuwa debeni, 2032 atakuwa na miaka 79.

Baadhi ya viongozi wa chama chake kutoka Ukambani wamekuwa wakisema kama hatakuwa debeni atasahaulika kwa sababu wapigakura watamchoka na kuanza kuwaunga viongozi chipukizi.

Baada ya kumaliza wa tatu katika uchaguzi mkuu wa 2007, Bw Musyoka aliunda muungano na mshindi Mwai Kibaki na kupokezwa nafasi ya kuwa makamu wa rais kati ya 2007-2013.

Licha ya Bw Kibaki na wanasiasa wa Mlima Kenya kuahidi kumuunga 2013, alichezwa baada ya Uhuru Kenyatta kukumbatiwa.

“Siku moja akielekea Kitui mwaka 2011, Kibaki alisimama mjini Machakos na kuambia umati kuwa alikuwa amefurahi kufanya kazi nami na sasa kilichobakia ni kusukuma ile ingine (akirejelea urais),” akasema Bw Musyoka kwenye kitabu chake Against All Odds.

Hata hivyo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano afisi ya rais wakati huo Isaiah Kabira alituma taarifa na kukanusha kuwa Kibaki alikuwa amemuidhinisha Bw Musyoka.

Tena kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013, Bw Kenyatta na Ruto walikuwa wameahidi kumuunga mkono Bw Musyoka iwapo wangezuiwa kuwania kutokana na kesi zilizowaandama ICC.

Watatu hao waliandaa mikutano ya pamoja ya amani nchini kupitia muungano wa G7 lakini Bw Kenyatta na Ruto wakahiari kumuunga Musalia Mudavadi kisha wakamtoroka tena na kubuni muungano wao.

“Tulikubaliana kuwa ningekuwa mwaniaji wa urais, Uhuru awe mgombeaji mwenza kisha Ruto Kiongozi wa wengi. Hata hivyo, nafikiri walibadili nia baada ya kuangalia idadi ya kura katika ngome zao na zangu,” akaongeza Bw Musyoka.

Kuelekea uchaguzi wa 2017, Bw Musyoka alifichua kuwa alikubaliana kumuunga mkono Raila Odinga 2013 ahudumu muhula mmoja awe alishinda au la kisha amuunge mkono kupitia CORD.

Hata hivyo, ujio wa Musalia Mudavadi na kubuniwa kwa Muungano wa NASA ulivuruga makubaliano yao na akaishia kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga tena, lakini wakabwagwa na Bw Kenyatta.

Wakati wa kampeni za kura ya 2022, Bw Musyoka alikataa kuunga mkono Raila akisema alikuwa amekiuka makubaliano waliyokuwa nayo kuwa mara hii angekuwa mpeperushaji wa bendera wa upinzani.

“Raila alikubali kuhudumu muhula mmoja kisha aniunge 2022,” akasema Bw Musyoka akifichua kuwa mkataba huo ulitiwa saini Aprili 30, 2017.

Kwa wakati moja aliapa kuwa hangemuunga mkono Raila akidai amemsaliti kisiasa ya kutosha.

“Nitakuwa mtu mjinga zaidi kumuunga mkono Raila 2022,” akasema Bw Musyoka mnamo Juni 16, 2021.

Baada ya kulambishwa sakafu na Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Musyoka alidai amesalitiwa tena baada ya Raila kumwacha kwenye upinzani na kuamua kufanya kazi na Rais Ruto.

“Sisi tunaamua kusimama na Gen Z na Wakenya tukiwa upinzani. Wale ambao waliondoka upinzani (Raila) na kujiunga na Zakayo (Rais Ruto) historia itawahukumu vikali,” akasema mnamo Machi mwaka huu, 2025.

Katika muungano huu mpya, wandani wa Bw Musyoka wanaona 2027 kama mwaka wake kwa sababu kuna hofu kwamba wafuasi wake Ukambani wamechoka kumuunga Raila na hawako tayari kumuunga mkono mwanasiasa mwingine.

Tayari wandani wa Bw Musyoka wanamwona Dkt Matiang’i kama tishio kwa uwanizi wake huku wakikosoa hatua ya Jubilee kutangaza itamuunga mkono hata kabla ya wawaniaji wengine kufanya maamuzi.

“Kama Uhuru alishindwa kumfanya Raila awe Rais wakati ambapo alikuwa kiongozi wa nchi, sasa ndiyo atamfanya Matiang’i awe rais baada ya kustaafu,” akauliza Seneta wa Makueni Dan Maanzo.