Wanaume 'singo' hutoa uvundo unaowavutia wanawake siku za hedhi – Utafiti
MASHIRIKA Na PETER MBURU
UTAFITI wa kushtua umebaini kuwa wanaume wasio na wapenzi hutoa uvundo mkali zaidi mwilini na wana mashavu yenye misuli, ikilinganishwa na wenzao walio na wapenzi.
Utafiti huo ambao ulihusisha wanaume kufanyishwa kazi ngumu, kisha wanawake kunusa makwapa ya shati walizovalia wakifanya kazi hiyo ili kubaini kama kulikuwa na tofauti za kiharufu ulionyesha kuwa jasho la wanaume ambao hawakuwa na wake ama wapenzi baina yao lilinuka sana ikilinganishwa na la wenzao wenye wapenzi.
Vilevile, wanawake waliowanusa walisema kuwa wanaume wasio na wapenzi walikuwa na misuli usoni, zaidi ya waliokuwa na wapenzi.
Utafiti huu ulifanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Macquarie nchini Australia, kubaini ikiwa kuna tofauti ya chembechembe za testosterone katika mili ya wanaume wenye wapenzi na walio ‘singo’.
Baadaye, matokeo yake yalichapishwa katika jarida la Frontiers in Psychology nchini humo.
Hata hivyo, utafiti huo uliendelea kusema kuwa hali hiyo inaweza kuishia kuwafaa wanaume hao wasio na wapenzi.
Wanawake 82 wanaojihusisha kimapenzi na wanaume walitumiwa kufanya utafiti huo wa kunusa jasho la wanaume hao, wote wakiwa kati ya umri wa miaka 18 na 35.
Baada ya wanaume kufanya kazi nzito, sehemu ya makwapa za mashati zao zilikatwa na kupewa wanawake hao kunusa na kueleza kiwango cha uvundo.
Utafiti huo ulionyesha kuwa wanawake hao walisema harufu ya jasho la wanaume wenye wapenzi ilikuwa kiwango cha 3, ilhali wale ‘singo’ kilikuwa 6.
Vilevile, wanawake hao walisema kuwa wanaume wasio na wapenzi walikuwa na nyuso zenye misuli kuliko wale walio katika uhusiano wa kimapenzi.
Utafiti huo si wa kwanza kubaini uhusiano baina ya kiwango cha chembechembe za testosterone mwilini na harufu anayotoa mtu.
Mwingine ambao ulichapishwa mnamo 2013 ulionyesha kuwa wanawake huvutiwa na wanaume walio na kiwango kikubwa cha testosterone, haswa wanapokuwa katika msimu wa hedhi. Wanaume hawa ndio hutoa na harufu nyingi mwilini.