Mabwanyenye, wanasiasa wapambana kuokoa mali isipigwe mnada
WAFANYABIASHARA wakubwa katika sekta mbalimbali kama vile utengenezaji wa bidhaa, usafirishaji wa mizigo, biashara ya kilimo, mali isiyohamishika, usindikaji wa chakula, uuzaji wa chai nje ya nchi na ujenzi, wamekuwa wakipambana kuzuia mali yao kuuzwa kwa mnada na taasisi za kifedha baada ya kushindwa kulipa mikopo.
Wafanyabiashara hao wakiongozwa na mwanzilishi wa Benki ya Equity, Peter Munga, David Langat wa DL Group anayehusika na biashara ya chai, mwanakandarasi Josiah Njoroge Njuguna wa kampuni ya Nyoro Construction, miongoni mwa wengine, wanazozana na benki tofauti katika juhudi za kuokoa mali yao isipigwe mnada.
Hata wanasiasa hawajasazwa katika msukosuko huu wa kifedha, kwani baadhi yao kama Mshauri Mkuu wa Rais wa Masuala ya Uchumi Moses Kuria, wabunge wa zamani Naomi Shaaban, Charles Kilonzo, na Swarup Mishra wamekuwa wakikwepa nyundo ya mnada isiwaangukie.
Katika sekta ya biashara ya kilimo na usindikaji, mfanyabiashara bilionea Peter Munga (mmiliki wa Equatorial Nuts Ltd, Murang’a) na aliyekuwa Mbunge wa Thika mjini Patrick Jungle Wainaina (mmiliki wa Jungle Macs EPZ, Thika) wanapinga kuuzwa kwa mali zao kutokana na mikopo inayohusishwa na kampuni zao.
Wiki iliyopita, Bw Munga alishindwa kuzuia Benki ya ABC kuuza hisa zake milioni 75 katika kampuni ya bima ya Britam Kenya, ili kurejesha mkopo wa Sh433 milioni uliokopwa na kampuni yake, Equatorial Nut Processors.